[caption id="attachment_26750" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Wilaya ya Chato Shabani Ntarambe (aliyesimama) akimweleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia) wakati wa mkutano wa hadhara kwenye soko la kimataifa la samaki la Kasenda wilayani Chato leo.[/caption]
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameamuru kufanyika ukaguzi mpya wa hesabu za fedha kwenye masoko yote ya kimataifa ya samaki na mazao yake yaliyoko katika Ziwa Victoria ili kuhakiki uhalali wa mapato ya Serikali yaliyokusanywa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Masoko hayo yatakayohusika na ukaguzi huo ni pamoja na Kirumba Mwanza, Nyakalilo Buchosa Mwanza, Kasenda Chato Geita, Magalini Muleba Kagera, Kemondo Bukoba Kagera na Mwigobero Musoma Mara ambapo wafanyabiashara watakaobainika walihusika kufanya udanganyifu wa mapato watatakiwa kurejesha fedha hizo walizoiibia Serikali kwa kipindi hicho.
Pia Watumishi wa Umma waliohusika kuhujumu mapato hayo watasakwa popote walipo na kufikishwa kwenye vyombo vya dola kukabiliana na mashtaka ya kuhujumu rasimali za nchi.
[caption id="attachment_26751" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia katikati) akiwa kwenye moja ya boti inayotumika kwa Uvuvi wa samaki kwenye soko la kimataifa la samaki la Kasenda wilayani Chato leo, Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chato Bathromeo Christiani, Kushoto ni Diwani wa kata ya Kasenda Muganza Mwita.[/caption]Hatua hiyo ya Waziri Mpina imekuja kufuatia kubaini kuwepo udanganyifu mkubwa katika biashara ya samaki, dagaa, mabondo, na mapanki akibainisha kuwepo tabia ya kupunguza uzito na idadi ya magunia, kubadilisha matumizi ya vibali, kuchanganya mizigo ya ndani na nje ya nchi kwenye malori, kuanzishwa kwa masoko ya kimataifa yasiyo rasmi na wafanyabiashara wakubwa wa mazao ya uvuvi kutolipa kodi za mapato kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pia Waziri Mpina ameamuru kufutwa kwa masoko yote yasiyo rasmi yaliyopewa hadhi ya kimataifa ikiwemo soko la Nyakalilo na Magalini ambapo amemuagiza Katibu Mkuu Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba kuwaondoa na kuwapangia vituo vingine vya kazi watumishi waliokuwepo kwenye masoko hayo.
Waziri Mpina ametolea mfano udanganyifu mkubwa uliofanywa na wafanyabiashara na watumishi wa umma wasio waaminifu likiwemo tukio la Disemba 16 mwaka jana ambapo mfanyabiashara mmoja (jina tunalo)huku akitumia gari lenye usajili ya nchi ya Rwanda lenye namba za usajili RB 9591 alipewa kibali cha kusafirisha magunia 258 kwenda Ngara mkoani Kagera na badala yake aliyapeleka nchini Rwanda na kuisababishia Serikali hasara ya sh. Milioni 3.
Pia kupunguza uzito na idadi ya magunia ili kulipia kidogo mapato ya Serikali akitolea mfano mfanyabiashara mwingine (jina tunalo) ambapo Disemba 2 , 2017 kutoka soko la Kasenda alisafirisha magunia 300 ya dagaa lakini yaliyolipiwa mrabaha wa Serikali ni magunia 200 tu huku Serikali ikipoteza mapato ya magunia 100 .
Waziri Mpina amesema matukio hayo ya udanganyifu aliyotolea mfano ni ya siku moja tu huku wafanyabiashara hao wakiwa na utamaduni wa kusafirisha zaidi ya safari nane kwa mwezi ambapo Serikali hupoteza mabilioni ya fedha za mapato kwa mwaka ambapo Samaki, dagaa, kayabo, mabondo, mapanki,furu wamekuwa wakiroroshwa kupitia mipakani na njia ya panya kwenda nchi za Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Malawi, Uganda na Kenya.
[caption id="attachment_26752" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye kofia) akiwahutubia wananchi kwenye soko la kimataifa la samaki la Kasenda wilayani Chato leo.[/caption]Amesema wafanyabiashara waliopewa leseni za kusafirisha mazao ya uvuvi nje ya nchi wamekuwa mawakala wa raia wa kigeni ambapo kazi ya kununua, kukusanya na kusafirisha hufanywa na wageni jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 kifungu cha 13 (14).
Kuhusu kasi ya Uvuvi haramu katika Wilaya ya Chato Waziri Mpina amesema taarifa zinaonesha kwa kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2017 zana haramu zikiwemo Timba, Kokoro,Katuri,Mitumbwi, yenye thamani ya sh milioni 525,207,000 vilikamatwa, kutaifishwa na kuteketezwa.
Ametumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kuacha uvuvi haramu huku akieleza kusikitishwa na namna watanzania hao wazawa walivyopoteza mitaji yao lakini akatangaza msimamo mzito.
“Nimesononeshwa sana na taarifa ya kuteketezwa kwa mitaji ya wafanyabiashara hao wazawa kwa sababu ya kujihusisha na uvuvi haramu lakini nataka kuwakikishia kuwa vita dhidi ya uvuvi haramu haina suluhu na kwamba sitamuonea haya wala huruma mtu yoyote atakayejihusisha na uvuvi haramu tutawashughulikia wote bila huruma kwani Serikali ya awamu ya tano imejidhatiti kukabiliana na uvuvi haramu kwa nguvu zote na bila kuchoka”alisema Mpina.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwanaidi Mlolwa alisema jukumu la kulinda rasilimali za nchi liko kikatiba hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kusaidia kulinda rasilimali hizo zisitoroshwe kwa manufaa ya nchi ya nyingine.
Amesema Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 kifungu cha 37 (a) (ii) na (iii) na kanuni zake za mwaka 2009 zinawapa mamlaka wasimamizi wa Sheria hiyo kumkamata mtu yeyote anayekutwa na samaki na mazao yake waliovuliwa kwa njia haramu na kutaifisha mali zote ikiwemo samaki, boti, mitumbwi na magari yaliyobeba samaki hao.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shabani Ntarambe amesema katika kukabiliana na uvuvi haramu wilaya kwa kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2017 imefanikiwa kukamata ,kutaifisha na kuteketeza zana haramu za uvuvi zikiwemo Timba, Kokoro,Katuri,Mitumbwi, yenye thamani ya sh. milioni 525.2 na kumhakikishia Waziri Mpina kuwa mapambano bado yanaendelea kukomesha kabisa uvuvi haramu