Na Mwandishi wetu MOI
Taasisi ya tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imepokea timu ya madaktari bingwa kutoka Serikali ya Jamhuri ya watu wa China ambao watatoa huduma za kibingwa katika Taasisi za MOI, MNH, JKCI na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) kwa kipindi cha miaka miwili.
Mnamo mwezi Septemba mwaka 2021, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya iliingia mkataba namba 26 wa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China, mkataba huo pamoja na mambo mengine ulijikita katika mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na kuleta madaktari bingwa kutoka China kutoa huduma katika hospitali za kibingwa hapa nchini.
Akizungumza katika hafla ya kupokea madaktari bingwa hao katika Taasisi ya MOI, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface amesema ujio wa madaktari bingwa hao ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za kibingwa ambapo pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa madaktari hao watafundisha wanafunzi.
“Ujio wa wataalamu hawa una tija kubwa kwa Taasisi yetu na kwa nchi kwa ujumla kwani watafanya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari bingwa wazalendo jambo ambalo litapelekea kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kisasa, pia watatoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi kwani moja ya malengo ya MOI ni kutoa mafunzo” Alisema Dkt. Boniface
Kwa upande wake kiongozi wa timu ya madaktari bingwa kutoka China, Dkt. Meng Yong amesema ni heshima kubwa kupata fursa ya kufanya kazi Tanzania na kuwahudumia watanzania kwa kipindi cha miaka miwili ambapo pia watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na madaktari bingwa wenzao wa Tanzania na kujifunza mambo mengi.
Muwakilishi wa Wizara ya Afya Tanzania, Dkt. Vumilia Liggyle amesema ushirikiano baina ya Serikali hizi mbili (Tanzania na China) ni wa kihistoria kwani una zaidi ya miaka 50 na umekuwa ukienziwa kizazi hadi kizazi jambo ambalo limekuwa likiwanufaisha wataalamu kwenda nchini China kupata mafunzo na madaktari bingwa kutoka China kuja hapa nchini kutoa huduma.
“Tumepokea jumla ya Madaktari Bingwa 11 kutoka China, watatoa huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa miaka miwili katika hospitali zetu za kibingwa za MOI, JKCI, MNH na hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya (MZRH), alisema Dkt. Liggyle.
Ujio wa madaktari bingwa hawa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinapatikana hapa nchini na kuifanya Tanzania kuwa kituo cha matibabu barani Afrika.