[caption id="attachment_29547" align="aligncenter" width="900"] Madaktari Bingwa wa MOI kwa kushirikiana na daktari kutoka India wakifanya upasuaji mkubwa wa kubadilisha kiungo cha nyonga kilichochakaa kwa kuweka kiungo bandia ,kama asingefanyiwa upasuaji huu hapa MOI Mgonjwa huyu angelazimika kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa[/caption]
Na Mwandishi Wetu
Madaktari Bingwa wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili kwa kushirikiana na daktari bingwa wa Mifupa kutoka hospitali ya Prashanth Chenai ya nchini India leo wamefanya upasuaji mkubwa na mgumu wa kibingwa wa kubadilisha kiungo cha nyonga (Complicated Total Hip Surgery) cha mgonjwa ambacho kimeharibika na hivyo kumsababishia mgonjwa kushindwa kutembea na kupata maumivu makali.
Upasuaji huo umefanywa na jopo la madaktari bingwa wanne ambao wameongozwa na Dkt Mani Ramesh Kutoka India na Dkt Samweli Kitugi Nungu wa MOI ambapo upasuaji huo umefanyika kwa ufanisi na kwa masaa matatu.
Akizungumza baada ya Upasuaji huo Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema ujio wa daktari kutoka India ni sehemu ya mkakati wa Taasisi ya MOI kuwajengea uwezo wataalamu wake kwa kupata mbinu mpya kutoka kwa wataalamu kutoka nchi mbalimbali. Ushirikiano kama huu
“Mtaalamu huyu amekuwa hapa kwetu kwa siku tano, naamini wataalamu wetu wamejifunza mbinu mpya za matibabu haya ya kibingwa ya nyonga na lengo letu ni kuhakikisha hakuna mgonjwa anayekwenda nje ya nchi kufuata matibabu ya aina hii. Pia, itasaidia kupunguza gharama za mafunzo’’. Dkt Boniface
Pia, Dkt Boniface amesema kwa sasa Taasisi ya MOI inawafanyia upasuaji wagonjwa 25-30 kwa mwezi idadi ambayo haijawahi kufikiwa toka taasisi ianze kutoa huduma hizi za kibingwa za nyonga mwaka 2003. Na malengo ni kufikia wagonjwa 100 kwa mwezi baada ya kuanza kwa vyumba vipya viwili vya upasuaji katika jengo jipya la MOI (MOI Phase III)
Kwa upande wake Dkt Mani Ramesh kutoka India amesema, hii ni mara yake ya pili kufika MOI, amefarijika sana kwa namna Taasisi ya MOI inavyotoa huduma zake kwa watanzania na pia ni shemu ya kubadilishana uzoefu.
‘‘Nimefarijika sana kwa siku tano nilizokaa hapa Tanzania, tumeshirikiana na kubadilishana uzoefu kwenye matibabu haya ya kibingwa ya Nyonga, binafsi naamini huu ni muendelezo mzuri wa ushirikiano kati ya MOI na hospitali yetu ya Prashant naamini nitarajea tena hapa’’ Dkt Ramesh
Taasisi ya MOI imeshawafanyia upasuaji huu mkubwa zaidi ya wagonjwa 1000 mpaka sasa na Taasisi inatarajia kufungua chumba kipya cha upasuaji wa nyonga ambacho kitakuwa maalum kwa wagonjwa hawa kwani mahitaji ni makubwa sana kwa sasa. MOI imeweza kufanikisha yote haya kutokana na Serikali ya awamu ya Tano kutoa fedha za kununulia vifaa tiba na kuboresha miundo mbinu kwa ajili ya kutolea huduma hizi.