Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imekutana na watekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP-AEP) na kufanya tathmini na kuweka mikakati ya kuhakikisha wasichana waliokatisha masomo wanaopata mafunzo kupitia mradi huo wanasoma hadi kufika elimu ya juu ili kufanikisha malengo ya mradi huo.
Akizungumza wakati wa warsha ya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa ‘SEQUIP’mjini Morogoro tarehe 24 Februari, 2023, Mkurugenzi wa TEWW, Dkt. Michael Ng'umbi, amewataka watekelezaji wa mradi huo kote nchini kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa mradi huo na amewataka wakufunzi, waratibu na wafanyakazi wa TEWW kuhakikisha kuwa wasichana ambao wanajiunga na vituo vya mafunzo kwa ngazi ya sekondari wanafanikiwa kufanya vizuri kwenye masomo yao na kukidhi vigezo vya kuendelea na masomo kwa ngazi za juu za kidato cha tano, vyuo vya kati hadi vyuo vikuu.
“Niwasihi wote mtambue kuwa fursa hii iliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wasichana hawa ni ya kipekee sana na tunao wajibu wa kuhakikisha walengwa wa mradi huu wananufaika ipasavyo na uwekezaji pamoja na rasilimali zilizotolewa kwa ajili yao,” amesema
Dkt. Ng`umbi amesema kupitia mradi wa SEQUIP, TEWW imefanikiwa kufanya ukarabati na ujenzi wa majengo mapya ya ofisi pamoja na madarasa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Kilimanjaro, Ruvuma, Rukwa na Iringa pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu 370.
Ametaja mafanikio mengine yaliyotokana na mradi huo kuwa ni uhuishaji wa mitaala ya masomo ya Uraia, Historia, Jiografia, Kiingereza, Kiswahili, Hisabati na Bailojia pamoja na uandaaji wa mitaala ya masomo ya Kemia na Fizikia ili kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya matakwa ya sasa katika soko la ajira.
Dkt. Ng`umbi ameongeza kuwa mradi wa SEQUIP pia umefanikisha kupatikana kwa gari jipya pamoja na vifaa vya TEHAMA ambavyo ni Kompyuta, printa, scanna na projekta ambavyo ni nyenzo mahsusi katika utendaji kazi.
Kwa upande wao washiriki wa warsha hiyo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikisha kurejesha ndoto za wasichana ambao walikatisha masomo yao ambapo utayari wa kuwapa nafasi ya kurejea shuleni ni mafanikio makubwa sana kwa jamii ya kitanzania katika kuikomboa dhidi ya ujinga.
Washiriki hao walibainisha changamoto mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo ikiwemo mtazamo hasi kwa jamii juu ya kurejeshwa kwa wasichana kuendelea na masomo na jamii kutotambua umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
TEWW ni watekelezaji wa Mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari kwa njia mbadala ambapo mradi huo unagharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia.
Mradi wa SEQUIP ulianza kutekelezwa mwaka 2021 na unalenga kuwezesha wasichana 12,000 waliokatisha masomo kuendelea na masomo ya sekondari ambapo hadi sasa jumla ya wasichana 5,490 wanaendelea na masomo kwenye vituo mbalimbali nchini.
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imeanzishwa na Sheria ya Bunge Namba 12 ya Mwaka 1975 ambayo pamoja na majukumu mengine katika kutekeleza utekelezaji wa mradi ya ‘SEQUIP’ TEWW inawajibika kuwarejesha wasichana wa kitanzania waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwepo ujauzito ambapo malengo yake ni kuhakikisha kati ya mwaka 2020 mpaka 2026 jumla ya washichana Elfu kumi na mbili (12,000) wamerejea.
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imeanzishwa na Sheria ya Bunge Namba 12 ya Mwaka 1975 ambayo pamoja na majukumu mengine katika kutekeleza utekelezaji wa mradi ya ‘SEQUIP’ TEWW inawajibika kuwarejesha wasichana wa kitanzania waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwepo ujauzito ambapo malengo yake ni kuhakikisha kati ya mwaka 2020 mpaka 2026 jumla ya washichana Elfu kumi na mbili (12,000) wamerejea.