Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mkurugenzi Msigwa, Mkurugenzi Oparah Wakubaliana Kuwajengea Uwezo Maafisa Habari/Uhusiano Kufanya Kazi Zitakazoitangaza Vyema Afrika
May 25, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Afrika, Bw. Emeka Oparah kando ya Mkutano wa 33 wa Maafisa Uhusiano Barani Afrika (APRA) unaoendelea Katika ukumbi wa JINCC Jijini Dar es Salaam.


Katika mazungumzo hayo, Msigwa na Oparah wamekubaliana kuongeza ushirikiano kati ya Airtel na Wadau wa Mawasiliano wa Tanzania kwa kuwa na mipango ya kujenga uwezo kwa Maafisa Habari na Uhusiano ili kuwawezesha kufanya kazi zitakazoitangaza vyema Afrika na kukuza fursa za haki ya kupata taarifa.


Pia, wamezungumzia baadhi ya changamoto zinazowakabili Maafisa Mawasiliano na Uhusiano ambazo zinahitaji majawabu kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo Serikali.


Wamewashauri Maafisa Habari na Mawasiliano nchi kuendelea kuwa wabunifu, kueleza vizuri habari zinazohusu Afrika na kuhamasisha uongezaji wa thamani kuhusu bidhaa zinazozalishwa Afrika yakiwemo mazao ya kilimo na mifugo ambayo yanazalishwa bila kutumia kemikali na yenye uasilia.


Maafisa Uhusiano wa Afrika kutoka nchi 24 za Afrika wanaendelea na mkutano wao wa Mwaka ulioanza jana tarehe 23 Mei, 2022 hadi tarehe 27 Mei, 2022 katika ukumbi wa JNICC Jijini Dar es Salaam.


Pamoja na mambo mengine, mkutano huo unajadili juu ya ustahimilivu wa Afrika dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoikumba dunia pamoja na uwezo wake wa kushindani katika masuala mbalimbali duniani hususani katika uchumi.


Washiriki wa mkutano huo wanabadilishana mbinu mbalimbali za mawasiliano na mikakati imara ya namna ya kuitangaza vyema Afrika nje ya mipaka ili iweze kunufaika na fursa mbalimbali duniani yakiwemo masoko ya bidhaa zinazozalishwa Afrika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi