Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mkurugenzi Mpya TPA Apewa Wiki Mbili Bandari ya Bagamoyo
Jul 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Meneja Miliki wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Alexander Ndibalema, akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupeleke Mwakibete (mwenye koti la Buluu), eneo lililotengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Bandari ya Mbegani, wakati Naibu Waziri alipotembelea eneo hilo, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, ametoa siku kumi na nne (14) kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuwasilisha ripoti ya vitu vyote muhimu vinavyohitajika kwa maboresho ya miundombinu katika Bandari ya Bagamoyo.

Akizungumza mara baada ya kukagua Bandari hiyo mkoani Pwani, Naibu Waziri Mwakibete, amesema kuboreshwa kwa Bandari hiyo kutarahisisha shughuli za utalii nchini na hivyo kukuza pato la wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

“Kwa kuwa eneo hili la Bagamoyo ni muhimu sana kwa utalii nampa Mkurugenzi Mkuu wa TPA wiki mbili alete watalaam hapa waangalie vitu muhimu vya kuboresha”, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na maboresho ambayo Serikali imejipanga kuyafanya kwa Bandari bado inaendelea na mkakati wake wa kurasimisha Bandari bubu zinazozunguka eneo la Bahari ya Hindi ili kuweza kupunguza biashara za magendo ambazo zimekuwa zikiendelea kufanyika bila usimamizi mzuri.

Naye, Meneja Miliki wa TPA, Ndibalema Alexander, amemuhakikishia Naibu Waziri Mwakibete kuwa TPA iko tayari na itatuma watalaam wa kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya maboresho ya miundombinu ya Bandari hiyo lengo likiwa ni kuongeza wigo wa mapato kwa Mamlaka na kuhakikisha wananchi wanapata huduma katika miundombinu bora.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Hassani Rajabu, ameishukuru Serikali kwa kutupia jicho Bandari ya Bagamoyo na kusema maboresho ya miundombinu yatakayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, itaongeza pato kwa kuwa itaongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani Pwani.

Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Pwani kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi