Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

WCF Yalipa Fidia  Sh. bilioni 49.4
Mar 22, 2023
WCF Yalipa Fidia  Sh. bilioni 49.4
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma akieleza utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma, Machi 02, 2023.
Na Jacquiline Mrisho

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alieleza kuwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), umefanikiwa kulipa fidia stahiki ya jumla ya Shilingi bilioni 49.44 kwa wakati kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi takriban wanufaika 10,454 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2015. 

Takwimu hizo zimetolewa leo Machi 02, 2023 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dkt. John Mduma wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kwa Waandishi wa Habari, jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Mduma amesema kwamba Serikali kupitia WCF imeleta mageuzi makubwa nchini kwani kabla ya kuanzishwa kwa WCF, malipo ya fidia nchini kwa mwaka mzima yalikuwa chini ya Shilingi milioni 200 lakini baada ya kuanzishwa kwa WCF malipo yanaongezeka mwaka hadi mwaka.  

“Hadi kufikia Juni 30, 2022, WCF imelipa mafao yenye thamani ya Shilingi Bilioni 44.61 kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko kubwa kwa kulinganisha na kipindi cha kabla ya kuanza kwa WCF, kwa hesabu zisizokaguliwa, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Desemba 2022, WCF ililipa mafao ya jumla ya Shilingi bilioni 6.19 kwa wanufaika 1,004 na hivyo kufanya wanufaika wa Mfuko toka kuanzishwa kwake kufikia 10,454 ambao wamelipwa jumla ya Shilingi Bilioni 49.44.” alisema Dkt. Mduma.

Mkurugenzi Mkuu ameongeza kuwa, Mfuko huo umekuwa ukilipa  pensheni kwa wanufaika ambapo kwa mwezi Juni 2022, wanufaika 1,114 walilipwa kiasi cha Shilingi milioni 231.39 kwa kweli mwezi huo.

Akizungumzia kuhusu Kusajili Waajiri Tanzania Bara, Dkt. Mduma amesema kuwa, kwa taarifa zisizokaguliwa, hadi kufikia mwezi Februari 2023, WCF ilikuwa imesajili jumla ya waajiri 29,978 ambapo amefafanua kuwa ongezeko kubwa la waajiri kujisajili na Mfuko katika kipindi cha Awamu ya Sita ni kutokana na hatua za makusudi za Serikali kuweka vivutio vya kufanya biashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya uchangiaji na kutoa msamaha wa riba.

Aidha, katika upande wa uwekezaji hadi kufikia  Juni 30,  2022, Mfuko umekusanya jumla ya Shilingi bilioni 241.48 toka kwenye mapato yatokanayo na uwekezaji ambapo kwa takwimu za hivi karibuni, WCF ilitengeneza Shilingi bilioni 69.86 katika mwaka wa fedha 2020/2021 na Shilingi bilioni 74.29 katika mwaka wa fedha 2021/2022. 

Vile vile Dkt. Mduma ameongeza kuwa, jumla ya mali za Mfuko hadi Juni 30, 2022 ni Shilingi bilioni 545.16 ambapo asilimia 89.76 ya uwekezaji wa Mfuko upo kwenye Hati Fungani za Serikali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi