Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma
Mkoa wa Mbeya wadhamiria kuongeza thamani mazao yanayozalishwa katika Mkoa huo ili kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda utakaosaidia kukuza uchumi wan chi na kutoa ajira kwa wananchi
Akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Amos Makala amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa dhana ya ujenzi wa Viwanda inatekelezwa kwa Vitendo .
“Mwishoni mwa mwaka huu tunatarajia kuwa na moja ya viwanda vikubwa vyakuongeza thamani mazao yetu yakiwemo mahindi kwa kuzalisha unga na kitaanza uzalishaji katika Mkoa wetu. Kwa sasa kinachofanyika ni kukamilisha ujenzi na ufungaji wa mitambo,” alisisitiza Makala.
Akifafanua Mhe. Makala amesema kuwa mkoa huo umepiga hatua katika kutoa huduma bora kwa wananchi ambapo asilimia zaidi ya 80 wanapata maji safi na salama katika mkoa huo.
Akizungumzia mikakati ya mkoa huo katika kukuza uchumi, Makala amesema ni pamoja na ujenzi wa bandari kavu, barabara kwa kiwango cha lami ambapo Wilaya zote katika mkoa huo zimeunganishwa na barabara za lami hali inayochochea shughuli za uzalishaji mali.
Aliongeza kuwa, tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa meli mbili zenye uwezo wa kubeba tani 1000 na zimeanza kutoa huduma katika ziwa Nyasa hali itakayokuza bishara kati ya Tanzania na nchi jirani na kuwanufaisha Wananchi wa pande zote.
Kwa upande wa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza kilimo ni pamoja na kuhakikisha kuwa Maafisa Ugani wanawajibika katika maeneo yao, kuwahudumia Wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili hali inayochochea kuongezeka kwa uzalishaji.
Mkoa wa Mbeya ni mkoa wa pili kwa kuchangia Pato la Taifa baada ya Dar es Salaam, hali inayochochea ukuaji wa uchumi katika Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Kipindi cha TUNATEKELEZA kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawashirikisha Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara na kueleza mikakati, sera na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikao yao.