Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali itaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha miundombinu yote ya usafiri na uchukuzi mkoani Kagera inajengwa kwa viwango vya juu ili kuchochea uchumi wa mkoa huo.
Akizungumza mara baada ya kuanza ziara ya siku tatu mkoani humo, Prof. Mbarawa amesema Mkoa wa Kagera ni mkoa muhimu kiuchumi kwa Taifa kwa kuwa uko pembezoni mwa nchi na unaiunganisha nchi ya Tanzania na Uganda, Rwanda na Burundi ambapo ni soko zuri kwa bidhaa mbalimbali toka nchini.
“Tumejipanga kuhakikisha kwamba usafiri wa majini, angani na barabarani katika mkoa huu hususani kwa njia zote zinazounganisha Tanzania na Nchi jirani unaimarishwa na matokeo yake mtaanza kuyaona siku za hivi karibuni”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha mipango yote iliyopangwa na Serikali mwaka huu mkoani humo inatekelezwa kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha katika miradi yote.
Prof. Mbarawa ameitaka TPA mkoani Kagera kutowabugudhi wafanyakazi katika bandari hiyo (makuli) ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.
Aidha, amesema kwa sasa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kitaendelea kutumika na kuboreshwa ili kiweze kutoa huduma wakati wote na kuitaka Serikali ya Mkoa wa Kagera kuhakikisha eneo lililotengwa kwa ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Omukajunguti linahifadhiwa kwa matumizi ya siku zijazo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuhakikisha barabara nyingi mkoani humo zinapitika wakati wote wa mwaka na kuwahakikishia kuwa mkoa huo utatoa ushirikiano kwa Wizara ili kuhakikisha miradi yote iliyopangwa kutekelezwa inakamilika kwa wakati.
‘Mhe. Waziri Mkoa wetu huu barabara zake zikifunguka na meli ya MV Mwanza ikianza kutoa huduma uchumi wa Kagera utaimarika na kuchochea uzalishaji wa mazao ya kilimo amesema Meja Jenerali Mbuge.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Prof. Faustin Kamuzora amemuomba Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara ya Omugakorongo - Murongo KM 110 unaotarajiwa kuanza hivi karibuni sehemu ya kwanza uanzie Kayanga ili kuleta urahisi katika utekelezaji wa mradi huo.
Prof. Mbarawa yuko Mkoani Kagera kukagua miradi ya sekta za Ujenzi na Uchukuzi inayoendelea mkoani humo.