Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mkataba Ujenzi Daraja la Kigongo Busisi Wasainiwa
Jul 29, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_45872" align="aligncenter" width="750"] Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale akisaini Mkataba wa ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza na Mwakilishi kutoka kampuni ya ujenzi ya China Civil Engeering Construction Coorporation, Zhang Jang, katika hafla iliyofanyika Makao makuu ya Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA, Jijini Dar es Salaam, wanaoshuhudia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe na Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jaffo.[/caption] [caption id="attachment_45873" align="aligncenter" width="750"] : Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale na Mwakilishi kutoka kampuni ya ujenzi ya China Civil Engeering Construction Coorporation, Zhang Jang, wakionesha nakala za mkataba wa ujenzi wa Daraja la Kigongo- Busisi mara baada ya kusainiwa, ujenzi wake utagharimu TZS. Bilioni 592.[/caption]

Na.Mwandishi Wetu –MAELEZO.

Hatimaye historia imeandikwa nchini Tanzania kwa kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza lenye urefu wa kilometa 3.2, ambao utagharimu jumla ya fedha za kitanzania Bilioni 592.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja hilo, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe, amesema mradi huo utatekelezwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania bila kutegemea fedha za wafadhili.

Waziri Kamwelwe alisema mradi wa Kigongo Busisi kama ilivyo miradi mingine ya kimkakati ulipigwa vita sana na baadhi ya watanzania na hata wahisani, amesema hata baadhi ya wanasiasa waliupinga wakidai ni mradi mkubwa sana kwa taifa na hauna tija kwa wakazi wa maeneo hayo na nchi kwa ujumla.

“Serikali hii ikiamua jambo inalivalia njuga na inahakikisha linakamilika kwelikweli , huu ni mkonga wetu watanzania na haijawahi hata siku moja mkonga ukamshinda tembo hivyo tunafanya na tutafanikiwa kwa sababu tunatumia fedha zetu wenyewe ili hao waliotukatisha tamaa washangae ” Alisema Waziri Kamwelwe.

Amesemakuwa ni wakati sasa kwa watanzania kutembea kifua mbele kwani sasa kodi zao zinatumika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo, ndio maana mradi huo mkubwa unaanza kutekelezwa, sambamba na miradi mingine kama ya umeme wa mto Rufiji pamoja na kuendelea kununua ndege mpya ili kuimarisha shirika la ndege.

Amesema wahisani wengi walikuwa na masharti kwamba wakikuletea fedha wanakuletea na mkandarasi wao, hivyo amesema kwa Tanzania ya sasa haitakubalika kwani kuna mgawanyo wa majukumu na wataalam wa mikataba, kuna wataalam wa manunuzi na hata washauri katika miradi mbalimbali hivyo serikali iko makini sana hasa katika masuala ya mikataba ili wasiingie mikataba ambayo itakuja kuwa kifungo kwa watanzania.

Waziri Kamwelwe amesema wakati wa ujenzi wa daraja kutakuwa na ajira za kudumu zaidi ya elfu moja na ajira zisizo za kudumu zaidi ya elfu kumi, kwakua fedha ni za watanzania ni wajibu wa serikali kuhakikisha fedha zinawanufaisha watanzania.

Hafla ya utiaji saini mkataba wa Ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi ulihudhuriwa pia na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jaffo , wakuu wa mikoa ya Mwanza na Geita, wabunge kutoka katika mikoa hiyo pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu.

Ujenzi wa daraja hilo unatekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation kwa kushirikiana na kampuni ya China Railway 15 Bureau Group , na linatarajiwa kuwa na urefu wa kilometa 3.2 pamoja na barabara zenye urefu wa kilometa 1.66. mkoa wa Mwanza.

Utiaji saini huo ulifanywa na Mhandisi Patrick Mfugale Mtendaji Mkuu wa Tanroads kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw.Zhan Jang kwa niaba ya makampuni ya China Civil Engineering Cooperation na China Railway 15 Bureau Group.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi