Mkandarasi anayejenga na kukarabati soko la Kariakoo Estim Construction Limited ametakiwa kuongeza kasi ya kukamilisha mradi huo ili taratibu za kuwarejesha wafanyabiashara zikamilishwe.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu ,Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatius Mativila mara baada ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi huo uliofikia asilimia 91 jijini Dar es Salaam jana (Oktoba 30,2023).
"Mradi wa ukarabati na ujenzi wa soko la Kariakoo hadi sasa umefikia asilimia 91 na utakamilika hivi karibuni ambapo tunategemea zaidi ya wafanyabiashara 3,500 wapate nafasi za kufanya biashara katika mazingira ya kisasa, hivyo serikali inataka kuona Mkandarasi akiongeza kasi ili mradi huu uwezeshe shughuli za kiuchumi kuendelea sokoni," alisema Mhandisi Mativila.
Mhandisi Mativila alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi bilioni 28.3 zilizofanikisha mradi huo ikiwa ni lengo la kuwajali wananchi wapate eneo bora na la kisasa la kufanyia biashara.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Sigsibert Valentine alisema maandalizi ya taratibu za kuwerejesha wafanyabiashara sokoni yanaendelea na utakuwa ni wa uwazi.
Mradi huo unatekelezwa kufuatia janga la moto lililotokea Julai 10, 2021 ambapo serikali imetoa shilingi bilioni 28.03 ili kufanikisha ujenzi na ukarabati ulioanza Januari 2022 na ulitarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu kupitia mkandarasi Estim Construction Limited ya Dar es Salaam na mtaalam mshauri akiwa ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).