Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mitambo ya Kurushia Ndege Tanzania ni ya Kisasa na Salama- Johari
Aug 25, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Grace Semfuko - MAELEZO

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA, Bw. Hamza Johari amesema mitambo yote ya kurushia ndege ya nchini Tanzania ni ya kisasa kabisa na inafanya kazi vizuri na kuihakikishia Dunia kwamba Tanzania ni salama katika ya anga.

Ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Shirikisho la Kimataifa la Wahandisi na Mafundi wa mitambo inayotumika katika kuongozea ndege- IFATSEA Kanda ya Afrika, ambapo amesema kuwa wahandisi na mafundi wanapaswa kuwa na mafunzo stahiki na endelevu ya uendeshaji wa mitambo hiyo.

Tanzania ni mwanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Wahandisi na Mafundi wa mitambo inayotumika katika kuongozea ndege- IFATSEA kupitia Shirikisho lao la Chama cha Wahandisi wa Mitambo ya Kuongozea Ndege Tanzania (TATSEA) ambapo kwa mara ya kwanza wamekuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa.

“Lengo lao Wahandisi na Mafundi hawa ni kuhakikisha mitambo hii wakati wote inafanya kazi vizuri, kusiwe na tukio kwamba mtambo fulani au rada fulani na ndege imezimika na haiwezi kwenda kwa sababu ndege bila mawasiliano haiwezi kufanya kazi, kwa hiyo wamekutana hapa na watajadiliana uzuri tu ni kwamba mitambo yetu mingi inafanya kazi vizuri na ni ya kisasa, jambo kubwa kwao mafundi wetu na Wahandisi wanapata mafunzo stahiki na endelevu kwa kadiri teknolojia inavyobadilika.” Amesema Bw. Johari.

Amesema mkutano huo ni muhimu kwa Dunia kwani utakuwa na mjadala muhimu wa usalama wa usafiri wa anga na kwamba wataalamu wanajadili yale ambayo yataboresha na kuimarisha sekta hiyo.

"Leo hapa unafanyika mkutano wa 12 wa Bara la Afrika wa Shirikisho la Wahandisi na mafundi wa mitambo inayotumika katika kuongozea ndege, sasa Wahandisi na Mafundi wana chama chao ambapo wanajadili mambo mbalimbali yanayohusu mitambo inayoshughulika na huduma za kuongozea ndege Duniani.” Amesema Bw. Johari.

Mkutano wa 12 wa Shirikisho la Wahandisi na mafundi wa mitambo inayotumika katika kuongozea ndege IFATSEA Kanda ya Afrika unafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania ambapo inatajwa kuwa kumekuwa na uimarishaji na uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafiri wa anga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi