Baadhi ya Wasanii waliokidhi vigezo vya kisheria na kukidhi masharti ya kupata mgawo wa mirabaha wameendelea kumiminika katika ofisi za Taasisi ya Hakimiliki (COSOTA), kuanzia jana Januari 31, 2022, kuwasilisha taarifa zao za kibenki na kukamilisha taratibu za msingi ili kuweza kukamilisha zoezi la ulipwaji wa mirabaha yao.
Miongoni mwa Wasanii hao ni Ambwene Yesaya (AY), Farid Kubanda (Fid Q), Chege Chigunda pamoja na Meneja wa kundi la Mabantu.
Pamoja na hayo, Wasanii hao wamemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuweka msisitizo katika kusimamiwa kwa Hakimiliki za Wasanii pamoja na kuhakikisha wasanii hao wanapata mgao wa mirabaha kwa kazi zao zinazotumika katika maeneo mbalimbali ya biashara.
Halikadhalika, wameipongeza COSOTA kwa kuwalipa mirabaha kwani ni muda mrefu hawajapata mirabaha na pia hawajawahi kupata gawio kubwa kama ilivyo katika mgao huo wa sasa.
Kwa mujibu wa Sheria, Wasanii wanaolipwa mirabaha ni wale ambao kazi zao wamejisajili COSOTA na pia kazi hizo zimethibitika kutumiwa kibiashara (economic use) kama vile muziki kupigwa katika vituo vya redio au kazi yoyote ya fasihi mfano kitabi kuingizwa katika matumizi ya kuigizwa katika filamu ya kibiashara.
“Mrabaha si mbadala wa mauzo ya kazi ya msanii bali ni kama fidia anayopewa mbunifu kwa kazi yake aliyoiingiza sokoni kisha kutumiwa na watu wengine kibiashara. Iwapo kazi ya msanii haijatumiwa kibiashara hata kama ameiuza na iko sokoni kwa wingi basi hana haki ya mrabaha na wingi wa kutumika kazi ya mtu ndio unaotofautisha ukubwa wa mapato kati ya mtu mmoja hadi mwingine,” amefafanua Ofisa wa Cosota.