Serikali kupitia Wizara ya Madini imedhamiria kuweka mikakati ya kuongeza ushiriki wa watanzania katika shughuli za madini ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watanzania wanaotoa huduma na usambazaji wa bidhaa migodini sambamba na kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine muhimu za kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde leo Januari 05, 2024 jijini Mwanza kwenye ufunguzi wa kikao na watoa huduma kwa wamiliki wa leseni za madini walioshiriki katika kikao hicho kilichohusisha pia Taasisi za Fedha, Vyama vya Wachimbaji wa Madini, Taasisi za Umma, Wizara ya Madini na Taasisi zake.
Aidha, amesema kuwa Wizara ya Madini kupitia Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri inatarajia kufanya utafiti wa kina wa madini nchi nzima utakaoondoa uchimbaji wa madini wa kubahatisha na kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Madini ikiwemo idadi ya kampuni kubwa za uchimbaji wa madini zitakazopelekea ongezeko la watoa huduma kwenye migodi ya madini, ushiriki wa watanzania na Sekta Binafsi.
“Dhamira ya Serikali kupitia Wizara Madini ni kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini, mapato ya nchi kuongezeka na kuwa Sekta inayoongoza katika mchango katika uchumi wa nchi,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Ameongeza kuwa, nia ya Serikali ni kuona watoa huduma wanazalisha bidhaa bora nchini na kuwataka kuungana na kuwa na nguvu ya pamoja kwenye uzalishaji ili kutosheleza mahitaji makubwa ya kampuni za madini nchini.
“Nipo hapa tuzungumze, kupromote uzalishaji wa bidhaa za ndani, lazima tubadilishe jambo hili, ni eneo ambalo nitalisimamia kwa dhati, vitu vingi bado vinaagizwa nje, tunaweza kuwajengea uwezo watu wetu ili wazalishe ndani na huu ndio utaratibu wetu sisi. Ninataka kuacha alama katika eneo hili, nipo tayari kupokea changamoto za kisheria na kikanuni na kuzifanyia kazi,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Kufuatia hali hiyo, ametoa rai kwa Taasisi za Fedha kuwawezesha watanzania kimitaji ili waweze kushiriki katika Uchumi wa Madini na kuongeza kwamba, Serikali ipo tayari kuwaonesha fursa zilizopo katika Sekta ya Madini na namna wanavyoweza kushiriki.
Pia amewataka wadau wa madini nchini kujipanga kwenye uwekezaji katika madini ya kimkakati kwa kuwa mahitaji yake yanaendelea kuongezeka duniani.
“Mfano mahitaji ya madini aina ya kinywe (graphite) yanatarajiwa kufikia asilimia 500 kwenye uchumi wa dunia ifikapo mwaka 2050 na madini haya tunayo, hivyo ni vyema tukaanza kujipanga kwenda kwenye uchumi shindani.” amesema Waziri Mavunde.
Awali, akielezea mafanikio ya utekelezaji wa Kanuni za Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini za mwaka 2018, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba ameeleza kuwa ni pamoja na ongezeko la ajira kwenye migodi kutoka 6,668 kati ya 7,003 ikiwa ni asilimia 95 mwaka 2018 hadi kufikia 16,462 kati ya 17,024 sawa na asilimia 97 kwa mwaka 2022 na ongezeko la manunuzi ya huduma na bidhaa kwa kampuni za kitanzania kutoka Dola za Marekani milioni 756.63 ambayo ni sawa na asilimia 62 ya manunuzi yaliyogharimu kiasi cha Dola za Marekani Milioni 1,228.38 kwa mwaka 2018 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.08 ambayo ni sawa na asilimia 86 ya kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.25 ya manunuzi yote yaliyofanyika mwaka 2022.