Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Migodi Mikubwa Yenye Ubia na Serikali Yachangia Trilioni 1.53 Kufikia Juni, 2023
Aug 21, 2023
Migodi Mikubwa Yenye Ubia na Serikali Yachangia Trilioni 1.53 Kufikia Juni, 2023
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali (aliyesimama) akielezea masuala mbalimbali kuhusu hali ya uendeshaji wa migodi ambayo Serikali ina hisa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo Agosti 21, 2023 jijini Dodoma
Na Wizara ya Madini

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa hadi kufikia Juni, 2023 miradi ya uchimbaji mkubwa wa madini ambayo Serikali ina hisa imechangia mapato ya Serikali ya jumla ya shilingi Trilioni 1.53 ambayo yametokana na tozo na kodi mbalimbali.

Mahimbali ameyasema hayo Agosti 21, 2023 jijini Dodoma kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya uendeshaji wa migodi ambayo Serikali ina hisa na mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inahuisha mikataba katika migodi mikubwa ili iendane na mabadiliko yaliyofanyika kwenye Sheria ya Madini pamoja na Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili, 2017.

Ameongeza kwamba, mbali ya kuchangia kodi, migodi hiyo imewezesha kutoa ajira zipatazo 3,110 kwa  watanzania na kuchangia kiasi cha shilingi 21, 045, 546,929.42 ikiwa ni mchango  kutokana na Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) pamoja na kutumia jumla ya shilingi 2, 893,423, 283, 326.05 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa na huduma nchini.

Ameitaja migodi hiyo  kuwa ni  North Mara, Buzwagi, na Bulyanhulu inayochimba madini ya dhahabu  kupitia   Kampuni ya Twiga Minerals Corporation Limited , kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya nikeli katika eneo la Kabanga wilayani Ngala, Faru Graphite Corporation Limited itakayojihusisha na uchimbaji wa madini ya Kinywe wilayani Mahenge na Mamba Minerals inayojihusisha na uchimbaji wa madini adimu yaani ( Rare Earth  Elements ) katika eneo la Nguala mkoa wa Songwe.

‘’Mhe. Mwenyekiti migodi mingine yenye hisa na Serikali iliyochangia mapato hayo ni kampuni ya Sotta Mining Limited kupitia mgodi wa Nyanzaga uliopo Wilayani Sengerema, na kampuni ya Williamson Diamond Limited (WDL) kupitia mgodi wa  Mwadui uliopo Mkoa wa Shinyanga.

Aidha, Mahimbali ameieleza kamati hiyo  kwamba,  katika kuhakikisha Serikali inanufaika  na uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini na kusimamia utekelezaji kulingana na matakwa  ya Sheria  ya Madini,  Serikali inatarajia kutoa leseni za uchimbaji wa madini kwa  kampuni za Duma TanzGraphite na Nyati Minerals Sand Limited zitakazofanya uchimbaji mkubwa pamoja na Kudu Graphite Limited  itakayofanya uchimbaji wa Kati na kuongeza kwamba, Serikali itakuwa na umiliki wa hisa za asilimia 16 kwa kila mradi.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mahimbali ameieleza Kamati hiyo mikakati ya Wizara kuiendeleza  Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inaifungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyinigne za kiuchumi na kuzitaja baadhi kuwa ni Kilimo ambapo rasilimali madini hutumika katika uzalishaji wa mbolea kwa matumizi ya kilimo. Aidha, ametumia fursa hiyo  kuishukuru kamati hiyo kutokana na ushauri na maelekezo  yake ambayo yameiwezesha  Sekta ya Madini kuendelea kufanya vizuri ikiwemo kupata tuzo tatu  zilizotolewa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Agosti  Agosti, 2023 kwa taasisi zilizofanya vizuri ambapo  Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya Twiga zilipata ushindi wa kwanza kupitia vipengele mbalimbali .

Akijibu hoja iliyotolewa na Kamati kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo  Dunstan Kitandula na wajumbe wengine la kuiwezesha STAMICO kusimama kwa niaba ya Serikali katika kampuni za uchimbaji mkubwa na wa kati  wa madini badala ya kuanzisha kampuni nyingine tanzu,  amesema kuwa Serikali imeyachukua maelekezo hayo na pia  wizara ina mpango  wa kuiwezesha STAMICO kuwa na ushindani na kampuni kubwa za nje ikiwemo kuiwezesha kuvuka mipaka ya ndani na kuwekeza katika mataifa mbalimbali  barani Afrika.

‘’ Mhe. Mwenyekiti suala hili litafuatiliwa kwa umakini na kwa kuzingatia taratibu, maelekezo haya ni dhabiti na yataongeza tija kwenye Sekta ya Madini.’’amesema Mahimbali.

Kuhusu suala la kuhakikisha miradi ya madini inatekelezwa hususan ile inayotarajia kuanza utekelezaji, amesema Wizara imeweka mazingira ambayo yatawasaidia wawekezaji kuweza kufanya shughulli zao kikamilifu kulingana na muda uliopangwa.

Akizungumza katika kamati  hiyo, Mwenyekiti Kitandula ameitaka Wizara kuendelea kuwajengea wajumbe wa kamati hiyo uelewa kuhusu shughuli na miradi inayotekelezwa na wizara na wadau ili kupata uelewa wa pamoja na kuiwezesha kamati hiyo kusimamia na kuishauri Sekta ya Madini kikamilifu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi