Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mifumo ya Usimamizi wa Mapato na Matumizi Yaboreshwa
Jun 06, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Abdulaziz Ahmeid, Mtwara

SERIKALI ya Awamu ya Tano imepongezwa kwa kuhakikisha kwamba mifumo iliyopo ya usimamizi inaboreshwa na kufanya kazi iliyokusudiwa ili kuweka wazi mapato na matumizi.

Wakizungumza katika mahojiano maalum , washiriki katika mafunzo  ya  mfumo wa Epicor  akiwemo Bw. Frank Chonya ambaye ni Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa alisema kwamba serikali imekuwa ikifanya vyema kuleta mifumo inayozuia ubadhirifu na wizi wa rasilimali za umma.

Alisema mfumo wa Epicor ulioboreshwa ambao wamekuja kujifunza ni miongoni mwa mifumo mizuri kwa sababu unasaidia kuhakikisha kwamba wahasibu wanafanya kazi yao vyema na ripoti inapatikana papo hapo kwa usahihi.

‘’ mfumo unahimiza kila kitu kuwekwa kwa usahihi ili ripoti iwe sahihi juu ya mipango, matumizi na fedha na mfumo huo unaongeza uwajibikaji kwa kuwa unaonwa na watu wote watoa huduma na wapokeaji wa huduma.Chonya Alifafanua hatua iliyofikiwa

Wengine waliozungumza ni Haji Mtitima, mweka hazina kutoka Nanyumbu ambaye anasema mafunzo hayo yanawajenga katika kuhakikisha kwamba wanatumia Tehama kutengeneza bajeti na pia mapato na matumizi.

Mtitima alisema kumekuwepo na mwanga mkubwa katika mfumo mpya ambao kwa sasa wanajifunza kwa kuwa unaunganisha mifumo yote na kusomeka kama mfumo mmoja.Akisisitiza ni hatua kubwa na maboresho yanaonekana......

Naye Masha Muhunzi Mhasibu halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu alibainisha kuwa matarajio aliyonanyo mafunzo hayo yatasaidia kuwa na ripoti kamili kila wanapotoa taarifa ya mwisho.

Kiongozi  wa Timu ya Fedha kutoka Programu ya Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3), Dk Gemini Mtei jana akimkaribisha katibu tawala mkoa wa Mtwara kufungua mafunzo ya siku nne juu ya usimamizi wa fedha za umma  Mradi unaotekelezwa kwa kusimamiwa na tamisemi chini ya ufadhili wa USAID  alisema kwamba mfumo huo huakisi  mapato kutoka ngazi ya mtoa huduma hadi kwa mwananchi ambaye anaweza kufuatilia makubaliano  mbalimbali.

Alisema kuna maboresho makubwa katika mfumo huo ili kuwezesha utekelezaji wa mipango mbalimbali kunafanikiwa na kwenda sanjari na uwazi na uwajibikaji.

Aidha Gemini alisema kwamba  mfumo huo pamoja na kuongeza uwazi utawafanya wakuu wa idara kutambua shughuli zinazofanywa na kupitia Epicor upo udhibiti na hakuna mtu anayeweza kufanya maamuzi ya pekee katika mfumo.

 Mfumo huo wa  Epicor 10.2 tayari umeshafungwa katika mikoa 13 lakini unafanyakazi nchini kote ambapo kwa sasa mafunzo yameanza katika  katika vituo sita tofauti huku halmashauri zote zikitakiwa kutumia mfumo huo.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa miaka mitano wenye lengo la kuboresha mifumo ya tehema, mifumo ya fedha, rasilimali watu ikiwamo mgawanyo wa watumishi na ushirikishaji wa watu.

Naye Desderi Wengaa ambaye ni Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Mawasiliano, PS3 anasema Epicor ni mfumo wa Marekani wa kihasibu ambao umefanyiwa marekebisho na Watanzania na kwamba mafunzo yanayoendeshwa yamelenga kuleta uelewa wa pamoja.

Alisema  vituo vya afya kwa sasa vinatengeneza mipango na bajeti yao na hivyo kuongeza uwajibikaji na kutwaa mahitaji halisi.

Aidha mpango huo umesaidia menejimenti ya fedha, mapato na matumizi huku kukiwa na kuboreka kwa huduma

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi