Na John Mapepele
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Isdor Mpango ametoa maelekezo nane ya kukuza na kukibidhaisha kiswahili duniani.
Maelekezo hayo ameyatoa leo Julai 7, 2022 kwenye kilele cha siku ya kwanza ya kiswahili jijini Dar es Salaam.
Amesema kuanzia sasa nyaraka zote za Serikali, dhifa na mijadala yote itafanyika kwa lugha ya kiswahili.
Aidha, ameongeza kuwa majina ya barabara na maelekezo ya dawa zote lazima yaandikwe kwa kiswahili ili wananchi wengi waweze kusoma na kuelewa.
Pia taarifa za miradi na mikataba yote ya Serikali lazima kuandikwa kwa kiswahili.
Kwa upande mwingine amesema Sheria na Kanuni ambazo bado hazijatafrisiriwa kwa lugha za kiswahili taasisi zinazohusika zishirikiane na Mwana Sheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Mpango amesisitiza kuwa Vyombo vya Habari lazima kuzingatia sarufi sahihi za lugha ya kiswahili.
Pia amefafanua kuwa agizo la awali lililotolewa na Serikali la kuzitaka Balozi zote za Tanzania kuanzisha vituo vya kujifunzia kiswahili na kuwatumia wataalam kutoka BAKITA na BAKIZA litekelezwe.
Pia amewataka BAKITA na BAKIZA kuwa wabunifu katika kubidhaisha lugha ya Kiswahili.
Aidha, ameelekeza mfumo wa kufundisha lugha ya Kiswahili kwa njia ya mtandao kutumika kikamifu.
Katika tukio hilo, Mhe. Mpango amezindua Mkakati wa Taifa wa kubidhaisha kiswahili, Kamusi ya Kiswahili na ametoa tuzo tatu ambapo ya kwanza imekwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa anaoutoa katika lugha ya kiswahili, na vyuo vya Ghana na Ujerumani.