Na Shamimu Nyaki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ametoa rai kwa Chama Cha Mpira wa Netiboli nchini (CHANETA) kuchagua wanamichezo wenye uwezo na weledi watakaounda timu ya Taifa ya mchezo huo.
Mhe. Gekul ametoa rai hiyo Novemba 03, 2022 katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro wakati akifunga Ligi ya Klabu Bingwa ya Muungano kwa mwaka huu ambayo imeshirikisha timu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
"Kwenye suala la kuchagua wachezaji wa timu ya Taifa nasisitiza mchague wachezaji wenye uwezo na sifa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mhe. Samia Suluhu inawekeza fedha za kutosha kwenye timu za Taifa, hivyo lazima muoneshe uwezo katika michezo ndani na nje ya nchi", amesema Mhe. Gekul
Ameipongeza CHANETA kwa nia yake ya kuendesha mafunzo ya Waalimu na waamuzi, huku akiagiza kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa kupata wadhamini wa kudumu katika ligi na maandalizi ya Kambi kwa timu ya Taifa.
Kwa upande wake Katibu wa CHANETA, Bi. Rose Mkisi amesema anaishukuru Serikali kwa ushirikiano inaotoa katika kuendesha mchezo wa Netiboli nchini.
Bi. Rose ameongeza kuwa, timu zilizoshiriki katika ligi hiyo ni 18, ambapo timu 12 ni za Wanawake na Wanaume timu 6 zote zikijumuisha Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwemo TAMISEMI QUEENS, KVZ, Mafunzo, Nyati Queens, Worriors Queens, JKT, JKU, Zimamoto, Bandari Veterans pamoja na Smart Boys.
Katika ligi hiyo TAMISEMI QUEENS wameibuka Mabingwa wa mwaka 2022, ambao pia ndio Bingwa mtetezi baada ya kuifunga timu ya Kikosi cha Valentia Zanzibar ( KVZ ) kwa jumla ya magoli 56 kwa 40.