Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mhe. Chande Awataka Watanzania Kuwa Wazalendo Katika Kutoa na Kudai Risiti za EFD.
Sep 26, 2023
Mhe. Chande Awataka Watanzania Kuwa Wazalendo Katika Kutoa na Kudai Risiti za EFD.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, akizungumza na wafanyabiashara wa Kata ya Kiusa, Wilaya ya Moshi Mjini, Mkoani Kilimanjaro, katika ziara ya siku mbili mkoani humo iliyolenga kutatua changamoto mbalimbali wanazopitia wafanyabiashara mkoani humo na kuhamasisha matumizi sahihi ya Mashine za Kieletroniki (EFD).
Na Joseph Mahumi, WF, Kilimanjaro

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, amewataka Watanzania kuwa wazalendo zaidi katika kutoa na kudai risiti ya mashine za Kieletroniki (EFD), ili kuhakikisha mapato ya nchi yanaongezeka na kusaidia kutekeleza miradi na huduma mbalimbali za kijamii.


 

Mhe. Chande, alitoa rai hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Kata ya Kiusa, Wilaya ya Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo iliyolenga kutatua changamoto mbalimbali wanazopitia wafanyabiashara mkoani humo na kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za Kieletroniki (EFD).


“Lazima Watanzania tuwe na utamaduni wa kudai risiti tunaponunua bidhaa na kutoa risiti tunapouza bidhaa, hii ndio chachu ya maendeleo ya nchi hii na itasaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo maji, shule na afya ifanyike kwa wingi” alisema Mhe. Chande.


 

Aliongeza kuwa, kila Mtanzania anapaswa kuwajibika katika kulipa kodi na kudai risiti halali ya kieletroniki kila wanapofanya manunuzi na ameitaka Mamlaka ya Mapato (TRA), kuhakikisha wanakusanya mapato halali bila usumbufu kwa wafanyabiashara.


 

Aidha, Mhe. Chande, amezindua kampeni kabambe ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ya “Tuwajibike” iliyobeba kaulimbiu ya “Kodi yetu, Maendeleo yetu” katika Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya EFD, ambayo imelenga kuhamasisha matumizi sahihi ya EFD ikiwakumbusha wauzaji kutoa risiti halali kila wanapofanya mauzo na wanunuzi kudai risiti halali kila wanaponunua bidhaa au kupata huduma. 


 

“Tuendelee kushirikiana kwa pamoja, na yule ambaye halipi kodi basi awe na utamaduni wa kulipa kodi kwa maslahi mapana ya Taifa letu na Serikali itawajibika kuleta maendeleo kwa wananchi wake, nanyi muwajibike kulinda na kuhifadhi miradi ya maendeleo inayoletwa na Serikali yenu” aliongeza Mhe. Chande.


Naye Mkuu wa Wilaya wa Moshi Mjini, Mhe. Kisare Matiku Makori, alisema kuwa wamekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya Ofisi za TRA na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ambao unasaidia kusogeza elimu ya mlipakodi karibu na wananchi.


 

“Nawaomba wananchi wangu wa Moshi muendelee kulipa kodi ili tuweze kufadhili miradi ya maendeleo na tumeona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anavyotuletea fedha za miradi hiyo” alisema Mhe. Makori.


 

Naye Meneja wa TRA mkoani humo, Bw. James Jilala, alisema kuwa Mapato ya Serikali ni muhimu, na mapato hayo kwa asilimia 61 yanatokana na makusanyo ya kodi na aliwasihi kutumia uzalendo katika kulipa kodi.


 

“Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23, tumevuka malengo kwa asilimia 102, hiyo ni kwa sababu ya jitihada za wafanyabishara wa Mkoa wa Kilimanjaro”

alisema Bw. Jilala.


 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi