Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mhe. Bashungwa Azielekeza Halmashauri Kutenga Fedha za Ujenzi wa Miundombinu ya Michezo
Sep 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Shamimu Nyaki

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa ametoa maelekezo kwa Mikoa na Halmashauri zote nchini, kutenga fedha kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo nchini.

Mhe. Bashungwa ametoa maelekezo hayo leo Septemba 16, 2022 Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa majibu ya nyongeza katika maswali ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu Serikali kujenga miundombinu na viwanja vya michezo.

"Ofisi ya Rais TAMISEMI inashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuendeleza sekta ya michezo ngazi ya Halmashauri, nasisitiza maeneo yote ya michezo katika shule zote za Msingi na Sekondari kupimwa na kutambua maeneo ya michezo na kuyalinda ili yasivamiwe", amesisitiza Mhe. Bashungwa.

Aidha, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akijibu swali la  nyongeza la Mhe. Sophia Mwakagenda kuhusu ujenzi wa miundombinu ya mchezo wa Masumbwi, amesema uwekezaji unaosisitizwa unajumlisha pia miundombinu ya mchezo huo.

Katika hatua nyingine, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azan Zungu ametoa pongezi kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiongozwa na Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu Waziri Pauline  Gekul,  Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi  na Naibu Katibu Mkuu, Saidi Yakubu kwa mapinduzi waliyofanya katika wizara hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi