Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mhasibu wa Mapori Arejeshwe kwenye Nafasi Yake - Majaliwa
Oct 09, 2018
Na Msemaji Mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Meneja wa Mapori ya akiba ya Buligi, Biharamulo na Kimisi Bw. Bigilamungu Kagoma amrudishe Mhasibu wa mapori hayo Bw. Adam Kajembe katika nafasi yake.

Ametoa agizo hilo baada ya Meneja wa Mapori hayo Bw. Kagoma kumuondoa mhasibu huyo  na kumteua Bibi Ruth Philemon ambaye ni Mhifadhi wa Wanyamapori kuwa mhasibu wa mapori hayo.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 8, 2018) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kwenye ukumbi wa JWTZ na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Biharamulo.

Waziri Mkuu amesema Meneja wa Mapori hayo hana mamlaka ya kuteua watumishi wa mapori hayo hivyo amemuagiza amuondoe haraka Bibi Ruth katika nafasi aliyompa na kumrudisha Bw. Adam kwenye nafasi yake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepiga marufuku wananchi kuingiza mifugo katika mapori ya akiba ya Biharamulo, Buligi na Kimisi.

Amesema mapori hayo kwa sasa yapo katika hatua za mwisho kutangazwa kuwa mbuga za wanyama, hivyo kuifanya wilaya hiyo kuwa miongoni mwa wilaya za kitalii nchini.

Waziri Mkuu amemuagiza Meneja anayesimamia mapori hayo, Bw. Kagoma ahakikishe mapori hayo yanalindwa na hakuna mifugo inayoingizwa.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, OKTOBA 8, 2018.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi