Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mhandisi Kundo Awapa Somo Wakuu wa Mikoa Kuhusu Anuani za Makazi.
Aug 27, 2023
Mhandisi Kundo Awapa Somo Wakuu wa Mikoa Kuhusu Anuani za Makazi.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akizungumza wakati akitoa mada kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala nchini waliokuwa kwenye mafunzo Kibaha mkoani Pwani,
Na Grace Semfuko- MAELEZO

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amewaambia Wakuu wa Mikoa kuwa zoezi la mfumo wa anwani za makazi limevuka lengo kwa kuongezeka kwa asilimia 12.8 ya matarajio ya awali ya asilimia mia moja na kuwaomba Wakuu hao kuendelea kulisimamia zoezi hilo endelevu.

Amesema kuna Mabadiliko Makubwa yaliyotokea kufuatia utekelezaji wa mfumo huo ambayo ni pamoja na Wananchi kupata faida nyingi kwa urahisi ikiwepo ya kupata, kutoa, kupokea na kufikisha huduma mahali stahiki na kwa wakati.

Akizungumza wakati akitoa mada kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala nchini waliokuwa kwenye mafunzo Kibaha Mkoani Pwani, Mhandisi Kundo amesema ipo haja ya Wakuu hao kusimamia na kulifanya zoezi hilo kuwa endelevu.

“Lakini kwa sababu haya yote yanafanyika katika Halmashauri, Wilaya na Mikoa, ni muhimu kwenu kuendelea kutusaidia katika Halmashauri mnazozisimamia kuhakikisha kuna fedha inayoendelea kutengwa kwa ajili kufanya zoezi hili liwe endelevu na faida kwa wananchi” amesema Mhandisi Kundo.

Aidha, amezitaja sababu zinazolifanya zoezi hilo kuwa endelevu ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya Maendeleo ikiwepo watu na ujenzi wa miundombinu.

“Sasa mtu anaweza akajiuliza kwanini kama tumemaliza hili zoezi kwa nini tunaendelea tena, mfumo wa anwani za makazi ni sehemu ya maisha ya Watanzania, ni sehemu ya maisha ya watu wote Duniani, tunapojenga barabara, tunapojenga nyumba, watu wanapozaliwa kunakuwa na mabadiliko ambayo ni lazima iwe na mkakati uendelezaji wa zoezi hili” amefafanua Mhandisi Kundo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi