Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mhandisi Kasekenya Awataka TAZARA Kujipanga Upya
Dec 30, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu - WUU

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ameitaka Menejimenti ya Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA), kubuni mikakati ya kibiashara inayoweza kutekelezeka na kupimika ili kuliwezesha shirika hilo kutoa huduma bora na kupata faida kama ilivyokusudiwa awali.

Akizungumza mara baada ya kukagua karakana Kuu za TAZARA jijini Dar es Salaam, Mhandisi Kasekenya amesema ni wakati sasa kwa kila mwenye dhamana katika TAZARA kufanya kazi kwa kuzingatia maono ya waasisi wa reli hiyo.

“Tunao mzigo wa kutosha wa kusafirisha kwa reli ya TAZARA hivyo hakikisheni mnakuja na mkakati wa kibiashara utakaowezesha kuwa na vichwa vya treni na mabehewa yanayokidhi mahitaji ya dunia ya sasa,” amesisitiza Mhandisi Kasekenya.

Amezungumzia umuhimu wa karakana zote zilizopo kufanya kazi kikamilifu ili kupunguza msongamano wa mabehewa na vichwa vya treni vinavyotakiwa kukarabatiwa.

Aidha, ameitaka menejimenti ya TAZARA kushirikiana na wafanyakazi katika hatua zote ili kuongeza ari ya kufanya kazi pamoja na kutoa huduma zenye tija na kuvutia wasafirishaji na abiria.   

Naye Naibu Mkurugenzi wa TAZARA, Mhandisi Christopher Shiganza amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya, kuwa TAZARA wamejipanga kuhakikisha wanapata vichwa vya treni na mabehewa ya kisasa ili kuongeza tija katika huduma hiyo.

Ameiomba Serikali kuboresha sheria ya TAZARA ili kuimarisha umoja baina ya nchi wanachama na kuleta tija na ufanisi mkubwa katika huduma za uchukuzi. 

Reli ya TAZARA inayoanzia Dar es Salaam, (Tanzania) hadi Kapirimposhi (Zambia), ilijengwa mwaka 1970 hadi 1975 kwa ushirikiano wa mataifa ya Tanzania na Zambia na imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na udugu kati ya mataifa hayo mawili, ikiwa ni juhudi za waasisi wa mataifa hayo Mwl. Julias Nyerere na Mzee Keneth Kaunda.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi