Na mwandishi wetu
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2020 umepungua hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 3.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2019.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma Kaimu mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bi Ruth Minja amesema kuwa hali hiyo inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2020 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia ,mwezi Desemba, 2019.
“ Kupungua kwa Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2020 kumechangiwa na kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Januari 2020”, alisisitiza Bi Minja
Akifafanua amesema kuwa bei za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Januari, 2020 ikilinganishwa na bei za mwezi Januari, 2019 ni pamoja na; dagaa kwa asilimia 1.4; viazi asilimia 3.4; magimbi asilimia 3.7 na ndizi za kupika kwa asilimia 2.8.
Kwa upande mwingine, baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizopungua bei kwa mwezi Januari, 2020 ikilinganishwa na bei za mwezi Januari, 2019 ni pamoja na ; gesi kwa asilimia 2.0; mafuta ya taa kwa asilimia 4.6; petrol kwa asilimia 1.5; dizeli kwa asilimia 1.3 na majiko ya gesi kwa asilimia 4.6.
Mfumuko wa Bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2020 umepungua hadi asilimia 5.7 kutoka asilimia 6.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2019.
Kwa upande wa nchi ya Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Januari ,2020 umepungua hadi asilimia 5.78 kutoka asilimia 5.82 kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2019. Kwa upande wa Uganda, Mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2020 umepungua pia hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2019.