[caption id="attachment_26543" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Desemba, 2017. Kulia ni Kaimu Meneja wa Takwimu za Bei na Ajira, George Milinga.[/caption]
Na Emmanuel Ghula
MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Desemba, 2017 umepungua hadi asilimia 4.0 kutoka asilimia 4.4 ilivyokuwa mwezi Novemba, 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kunatokana na kupungua kwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Desemba, 2017 ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwezi Novemba, 2017.
“Mfumuko wa Bei wa Taifa umepungua kutoka asilimia 4.4 mwezi Novemba, 2017 hadi kufikia asilimia 4.0 mwezi Desemba , 2017 kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma,” amesema Kwesigabo.
Mkurugenzi huyo amesema baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na unga wa muhogo uliopungua kwa asilimia 1.9, nyama kwa asilimia 3.4, samaki kwa asilimia 15.1, karanga kwa asilimia 3.5, mbogamboga kwa asilimia 2.9, njegere kwa asilimia 7.5, viazi mviringo kwa asilimia 6.7, mihogo mibichi kwa asilimia 16.8 na viazi vitamu kwa asilimia 12.5.
Amesema Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 109.21 mwezi Desemba, 2017 kutoka 108.94 mwezi Novemba, 2017.
Kwesigabo amesema Mfumuko wa Bei kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa mwezi Desemba, 2017 umepungua hadi asilimia 6.7 kutoka asilimia 7.9 mwezi Novemba, 2017. Huku Mfumuko wa Bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwezi Desemba, 2017 ikipungua kidogo hadi asilimia 1.3 kutoka asilimia 1.4 mwezi Novemba, 2017.
Amesema wastani wa Mfumuko wa Bei wa Taifa (kutoka Januari hadi Desemba, 2017) uliongezeka hadi asilimia 5.3 mwaka 2017 kutoka wastani wa asilimia 5.2 ilivyokuwa mwaka 2016 (kutoka Januari hadi Desemba, 2016). Kuongezeka kwa wastani wa Mfumuko wa Bei wa Taifa kulichangiwa hasa na kuongezeka kwa kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula. Wastani wa Mfumuko wa Bei wa bidhaa za vyakula uliongezeka hadi asilimia 9.6 mwaka 2017 kutoka asilimia 7.6 mwaka 2016.
Kwesigabo amesema Mfumuko wa Bei nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Desemba, 2017 umepungua hadi asilimia 4.50 kutoka asilimia 4.73 mwezi Novemba, 2017 na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 3.3 mwezi Desemba, 2017 kutoka asilimia 4.0 mwezi Novemba, 2017.