Mchengerwa Ampongeza Simbu Kutwaa Medali ya Fedha Jumuiya ya Madola
Jul 30, 2022
Na
Jacquiline Mrisho
Na John Mapepele, Uingereza.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amempongeza mwanariadha Alphonse Felix Simbu kwa kushika nafasi ya pili na Hamis Mesai kushika nafasi ya nane kwenye mashindano ya mbio za Marathoni ya Jumuiya ya Madola yanayoendelea nchini Uingereza.
Mhe. Mchengerwa amesema kazi ushindi Simbu ni wa watanzania wote ambapo amewataka wanamichezo wote wanaoshiriki mashindano hayo kutanguliza uzalendo ili kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Dkt. Asha-Rose Migiro akiwa na timu ya Taifa ya Riadha pamoja na mwanariadha Alphonce Felix Simbu baada ya kushinda medali ya Fedha kwa kuibuka mshindi wa pili mbio za marathon katika Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Birmingham, Uingereza, nyuma ya Victor Kiplagat wa Uganda leo. Mkimbiaji Hamisi Misai (wa tatu kulia) alimaliza katika kumi bora ya mashindano hayo kwa kushika nafasi ya nane. Wa pili kutoka kushoto ni Failuna Matanga ambaye alimaliza mtu wa tano katika marathon ya wanawake wakati Jackline Sakilu (wa pili kulia) akimaliza mwishoni akichechemea kutokana na maumivu ya msuli aliyoyapata akiwa kilomita 17 tu ya mchuano huo. Hivyo alichechemea hadi akamaliza huku akishangiliwa sana na umati mkubwa wa watu uliokuwepo. Kushoto ni kocha mkuu Suleiman Nyambui na kulia ni kocha msaidizi Lwiza John
Kufuatia ushindi huo Simbu anajinyakulia zawadi ya dola za kimarekani 7500 kutoka Serikalini ikiwa ni ahadi aliyoitoa waziri Mchengerwa wakati akiiaga timu ya Tanzania.
Mara baada ya kushinda Simbu amesema anawashukuru watanzania kwa maombi yao ambayo yamemfanya ashinde katika mashindano hayo.
Amesema siri ya ushindi ni mazoezi ambapo amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mchengerwa kwa kutoa msukumo wa pekee kwenye michezo.