Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mawasiliano Yainua Uchumi wa Wananchi wa Gairo
Jul 19, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mkuu wa Wilaya ya Gairo iliyopo Mkoani Morogoro Mhe. Sirieli Mchembe amesema kuwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye Wilaya hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa wananchi wake

Mhe. Mchembe ameyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea wilayani humo kwa ajili ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwa wote kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa makampuni ya simu, maeneo yaliyopo mipakani na yenye changamoto ya kijiografia kwa uwepo wa milima na mabonde kama ilivyo katika wilaya hiyo.

Ameongeza kuwa wananchi wake katika vijiji mbali mbali wanapata huduma za mawasiliano ikilinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali. Amefafanua kuwa mawasiliano yamefungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wake ambapo sasa wanaweza kuwasiliana na kufahamu bei ya mazao katika masoko mbali mbali nchini kwa kuwa wilaya hiyo inazalisha mazao ya biashara ya aina mbali mbali, kupata huduma za ulinzi na usalama kwa haraka na kwa wakati, kurahisisha utoaji wa taarifa zinazohusu afya za wananchi na upatikanaji wa huduma za matibabu na kuwawezesha wanafunzi na waaalimu kujifunza na kufundishia. Mhe. Mchembe ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za mawasiliano ambapo zimefungua fursa mbali mbali.

Akiongoza ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Selemani Kakoso ameipongeza Serikali kwa kujenga miundombinu ya mawasiliano kwa wananchi waishio wilayani Gairo kwa kuzingatia changamoto ya kijiografia ya eneo hilo ambapo sasa wanachi wanaweza kuwasiliana.

Kakoso amezitaka kampuni za simu kuzipatia Serikali za vijiji mapato yanayotokana na uwepo wa minara ya mawasiiano kwenye vijiji hivyo sehemu mbali mbali nchini ili mapato hayo yawawezeshe wananchi kunufaika nayo kwa kuwekeza kwenye masuala mbali mbali yanayogusa wananchi kama vile elimu na afya. Pia, amewataka kampuni za simu za mkononi kuweka minara yenye nguvu ya kutosha ili wananchi wapate mawasiliano wakati wote wa majira ya mwaka mzima na nyakati za usiku na mchana.

Mhe. Kakoso ametoa rai kwa wananchi kutunza minara kwa kuwa ni mali yao ambapo hapo awali walikosa huduma hiyo na baadhi yao kupoteza uhai. Amesema kuwa, “tumieni nafasi hii kuwekeza kwenye kilimo ili kutafuta masoko kwa kuwa Serikali imetengeeza miundombinu ya mawasiliano na baraara kwa ajili yenu”.

Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye kwa kushirikiana na Mhe. Kakoso na wajume wa Kamati wamezindua mnara wa mawasiliano uliopo kwenye kijiji cha Kumbulu kilichopo wilaya ya Gairo mkoani Morogoro ambao umepewa ruzuku na Serikali kupitia UCSAF ya kujenga mnara huo. Pia, uzinduzi huo umeshuhudiwa na Mhe. Nchembe, viongozi mbali mbali wa Serikali wa Wilaya hiyo na kamati ya ulinzi na usalama na wananchi waishio humo. Pia, ameilekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanza kufuatilia gharama za mawasiliano kwa kuwa wananchi wanaibiwa kwa kupiga simu tofauti na muda wa maongezi walionunua kwa kuwa kuna baadhi ya kampuni za simu wanafanya ulaghai kwa wananchi.

Pia, ameuelekeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilete kompyuta tatu na vifaa vyake kwa kila shule kwenye shule tatu za Kata ya Chanjale iliyopo wilayani Gario mkoani Morogoro ili kuwawezesha wanafunzi na waalimu kusoma na kufundishia kuendana na hali ya jiografia ya eneo hilo na ukuaji wa Teknolojia ya Habari a Mawasiliano duniani. Mhandisi Nditiye amewaeleza wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli iko tayari kuwahudumia wananchi na itaendelea kuwahudumia

Mtendaji Mkuu wa UCSAF Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa tayari UCSAF imefikisha mawasiliano kwenye kata 530 sehemu mbali mbali nchini ambapo Serikali imezipatia ruzuku kampuni hizo kujenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara na yenye cangamoto za kijiografia kama ilivyo kwenye Wilaya ya Gairo ambapo baadhi ya maeneo yana milima na mabonde hivyo upatikanaji wa mawasiliano hapo awali ulikuwa ni changamoto.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mnara huo, Meneja wa Kanda wa kampuni ya TIGO Bwana Joseph Mutalemwa ameishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku ya kujenga minara ya mawasiliano ili kuweza kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa sababu wao wenyewe wasingeweza kujenga minara hiyo. Pia, ameongeza kuwa wako tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kufikisha mawasiliano kwa wananchi kwenye sehemu mbali mbali nchini. Aidha, amefafanua kuwa uwepo wa mawasiliano kwenye maeneo hayo unatoa ajira kwa wananchi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi