Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amelipongeza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa hatua kubwa iliyopigwa katika kipindi kifupi kutoka kuwa Shirika tegemezi na kuwa Shirika linalojitegemea huku akilitaka kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kufikia azma ya kuwepo kwa Shirika hilo.
Ameyasema hayo jana jijini Dodoma katika kikao kifupi na Menejimenti ya Shirika hilo ambapo ameeleza kuwa STAMICO imefanya kazi kubwa katika muda mfupi na kuleta ushindani dhidi ya kampuni kubwa zilizokuwa zimezoeleka katika Sekta ya Madini hapa nchini.
“Nimpongeze Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Venance Mwasse tangu amefika hapa amefanya mapinduzi makubwa lakini bila ninyi asingeweza peke yake, nawapongeza sana na hiki kiwe kichocheo cha kufanya vizuri zaidi” amesema Waziri Mavunde.
Ameongeza “Lakini kwa upekee sana nimpongeze Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara, Kheri Mahimbali kwa usimamizi wao thabiti bila wao yawezekana msingefika hapa na nyinyi wenyewe mmekiri kuwa Wizara imewasaidia sana kufanya mapinduzi haya makubwa”.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo alimpongeza Waziri Mavunde kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Madini na kumuahidi kuwa Shirika litafanyia kazi maelekezo yake ili kufikia lengo.
Akizungumzia Mipango ya Shirika hilo, Meneja Rasilimali Watu Deusdedith Magala alieeleza kuwa Shirika limepanga kuondokana kabisa na utegemezi wa mishahara kutoka Serikalini kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 kuongeza gawio lake Serikalini mwaka 2024/2025, kuzalisha kwa wingi mkaa mbadala uonaotokana na makaa ya mawe na kuimarisha uchimbaji wa makaa ya mawe.
“Mhe. Waziri, Shirika limepanga kutekeleza Mkakati wake wa kuendeleza Wachimbaji Wadogo nchini sambamba na kutekeleza mpango wa mafunzo kwa ajili ya kutoa elimu kwa Wachimbaji mikoa yote nchini, kuongeza uwezo wa vituo vya mfano na kuendeleza ujenzi wa vituo vipya vya Lindi na Tanga, kuwasaidia kupata vifaa, na kuwaunganisha na wadau husika pamoja na kufanikisha zoezi la kuanzisha benki ya Wachimbaji nchini" amesema Magala