Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amebainisha vipaumbele vyake katika Sekta ya Madini ili kuhakikisha taifa linanufaika na uwepo wa Madini yanayopatikana hapa nchini huku akitaja Maono ifikapo mwaka 2030 kuwa madini ni Maisha na Utajiri.
Amebainisha hayo leo septemba 11 , 2023 wakati akizungumza katika Mkutano na Wachimbaji Wadogo wa madini kutoka Shirikisho la Wachimbaji wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika jijini Dodoma.
Akizungumzia juu ya kuongeza taarifa za utafiti wa jiolojia Mhe. Mavunde amesema moja ya vipaumbele vyake katika sekta ya madini ni kuijengea uwezo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili iweze kufanya utafiti wa kina kwa ndege yaani (Air Born Geophysical Survey) utakaotoa taarifa zitaonesha utajiri wa madini yaliyopo nchini kwa kiwango kikubwa tofauti na sasa ambapo ni asilimia 16 tu ya eneo lote nchi nzima limefanyiwa utafiti wa kina.
Waziri Mavunde amesema GST inapaswa kufanana na taasisi zote za Utafiti wa Madini duniani ikiwa na maabara ya kisasa itakayotumiwa na wachimbaji wote nchini.
“Ndugu zangu tukipiga picha ya miamba yote nchi nzima, tutapata taarifa sahihi ya kijiolojia ili wachimbaji wasifanye kazi zao kwa kubahatisha , uchimbaji ni Sayansi sio bahati wala uchawi, mchimbaji mwenye taarifa ya utafiiti wa kijiolojia atafanikiwa zaidi kupitia Sekta hii ya Madini,”amesema Mhe. Mavunde.
Aidha, ametaja mpango mwingine kuwa Wizara itaenda kuwa na makumbusho ya madini ili wananchi wapate kuona na kufahamu madini yanayopatikana nchini kuliko kuyasikia tu.
Akizungumzia kuhusu utoroshaji wa madini Mhe. Mavunde ametaja mkakati wa kutokomeza utoroshaji wa madini nchini ili madini yote yaliyopo kwenye mnyororo wa biashara ya madini yaonekane na yalete faida kwa taifa.
Amesema kuwa mtihani wake wa kwanza kama Waziri wa Madini ni kuhakikisha Wizara inakusanya shilingi trilioni 1 kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 hivyo suala la utoroshaji madini halina nafasi.
“Kuhusu utoroshaji naomba tushirikiane ntasimamia sheria, sitasita kuwachukulia hatua wale wote wanatorosha madini, sitaangalia sura ya mtu, mtahakikisha nasimamia kwa dhati na naamini kwa kushirikiana tutafanikisha kumaliza kabisa hilo tatizo, mimi na wenzangu tutakuwa wakali sana katika hili, milango yangu itakuwa wazi tushirikiane,” amesema Mavunde.