Serikali imesema kuwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu, Wamiliki wote wa mabasi watatakiwa kukatisha tiketi kwa njia ya kielekroniki kwa mabasi yaendayo mkoani ikiwa ni utekelezaji wa mikakati ya kuboresha utoaji huduma hizo kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dodoma, Katibu Mkuu- Uchukuzi, Gabriel Migire amesema nia ya kuanza utaratibu huo ni pamoja na kuthibiti Mapato yanayopatikana kwa njia ya tiketi na kuwarahisishia wamiliki kwa kujua idadi ya tiketi zilizouzwa kwa siku.
“Changamoto zote zilizowasilishwa awali na wadau zimerekebishwa kupitia Mamlaka Udhibiiti Usafiri Ardhini (LATRA) hivyo kukamilika kwa marekebisho haya Kutafanya zoezi hilo kuanza mwezi Julai”, Alisema migire.
Katibu Mkuu Migire amesema kwa sasa LATRA itaanza na majaribio kwa miezi mitatu ili kujiweka sawa na endapo itabainika kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo zitakamilishwa ili Julai uanze rasmi.
Karibu Mkuu Migire ameelezea faida za mfumo kwa abiria ikiwemo kutolazimika kwenda stendi ili kukata tiketi hivyo kumpunguzia adha ya kutafuta wakala kwani tiketi yake ataipata kupitia simu yake ya kiganjani.
Aidha, ameongeza kuwa kwa abiria wasiokuwa na simu janja watapata tiketi hizo kupitia mawakala wa mabenki ili kuwapunguzia kadhaa ya kutafuta mawakala walio katika stendi za mabasi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa LATRA, Giliard Ngewe amesema mamlaka itaanza kutoa elimu kuanzia Aprili Mosi ili kuwapa abiria uelewa wa namna ya kukata tiketi hizo kwa kuzingatia Makundi yote ya jamii.
Ngewe ameongeza kuwa elimu hiyo imeshirikisha taasisi zote muhimu ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania pamoja na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) ili kufikia watumiaji kwa haraka.