Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Matumizi ya TEHAMA Kunufaisha Taifa - Waziri Nape
Oct 28, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Chedaiwe Msuya, Zanzibar

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema ili kuharakisha mabadiliko ya kidijiti kwenye jamii ni lazima kuongeza usalama wa kimtandao pamoja na kupeleka huduma za mawasiliano zenye gharama nafuu kwenye jamii yote nchini.

Akifunga mkutano wa 6 wa mwaka wa TEHAMA Tanzania leo 28 Oktoba, 2022 Zanzibar Waziri Nape amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeainisha bayana namna ya kutumia teknolojia ya TEHAMA kwa maslahi mapana ya Taifa na watu wake.

“Ilani ya CCM imesema ni vema kutumia Teknolojia ya TEHAMA na kuthibiti hatari zinazotokea kutokana na mabadiliko ya teknolojia mpya za kidijiti pamoja na kurahisisha huduma mbalimbali za Serikali kwa umma, ili kuongeza kuzalisha vituo vya huduma kwa mteja”, amezungumza Mhe. Nape.

Aidha, Waziri Nape amewataka wataalamu wa TEHAMA kutumia muda wao kujifunza mbinu, kubuni mifumo inayoendana na mabadiliko chanya katika sekta ya mawasiliano. Hilo likifanyika, wageni watahamasika kuja kujifunza ndani na kubadilisha a uzoefu wa nchi walizotoka kupitia kongamano kama hili.

Awali akitoa salamu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa mjini Magharibi Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema mustakabali wa uchumi unategemea kwa kiasi kikubwa kasi ya kuwajibika na kujibadilisha utendaji wa kazi kidijiti.

“Kongamano la sita la mwaka la TEHAMA Tanzania 2022 limekuwa chachu ya kusukuma mabadiliko katika sekta ya TEHAMA,” amezungumza Mhe. Idrissa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema nia ya Serikali ni kuifanya TEHAMA kuwa na mchango mkubwa katika maswala ya Elimu na Utaalamu katika fani mbalimbali ili Mtanzania anufaike ipasavyo na huduma za TEHAMA nchini.

“Wito wangu kwa wana TEHAMA ni kwamba kile kidogo tulichonacho tujivunie ikiwemo kongamano la 6 la mwaka 2022 na tutafute fursa ili tutoke nje ya mipaka ya nchi yetu maana wenzetu hawana hiki tulichonacho ili nacho kichagize katika uchumi wa kidunia,” amezungumza Dkt. Yona.

Kongamano la 6 la mwaka la TEHAMA Tanzania 2022 (TAIC-2022) limefanyika Zanzibar kwa muda wa siku tatu kwa lengo la kuibua michango mbalimbali yenye kuonesha jinsi sekta ya TEHAMA inavyoweza kuchangia maendeleo ndani ya uchumi wa buluu na uchumi wa kidijiti, ambapo kongamano hilo limeongozwa na kauli mbiu isemayo “Mabadiliko ya Kidijiti kwenye uchumi wa buluu kwa maendeleo ya jamii na kiuchumi”.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi