Na Shamimu Nyaki - WUSM
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Jenista Muhagama amewagiza waandaaji wa Mashindano ya Wizara, Idara, Wakala na Mikoa (SHIMIWI) kuhakikisha watumishi wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu mashindano hayo.
Mhe. Mhagama ametoa agizo hilo leo Oktoba 05, 2022 Jijini Tanga, wakati akifungua michezo hiyo ambapo amesema kuanzia mwakani ziwepo timu mbalimbali za michezo kwa watu wenye uhitaji maalumu.
"Nitumie nafasi hii kuwahamasisha Watumishi wa Umma kushiriki mashindano haya, mwakani naomba idadi ya Waumishi iongezeke zaidi na michezo mingi ifanyike na muda wa kucheza michezo hii pia uongezwe ili Watumishi Washiriki kikamilifu haki hii ya msingi," amesema Mhe. Mhagama.
Mhe. Mhagama amewagiza waajiri wote nchini kuhakikisha wanamichezo wanawezeshwa vyema kushiriki michezo hiyo, huku akitaka wanamichezo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za michezo pamoja na Utumishi wa Umma.
Katika Hatua nyingine, Mhe. Mhagama amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma, ikiwemo upandaji wa madaraja, ubadilishaji wa kada na kufuta tozo ya thamani ya Mkopo wa Elimu ya Juu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Omary Mgumba, amesema usalama na huduma mbalimbali kwa wanamichezo katika mkoa huo umeimarishwa na wanamichezo wanaendelea kupata huduma kwa muda wote watakapokua mkoani hapo.
Jumla ya Timu 63 kutoka wizara 27, Mikoa 18, Idara za Serikali 18 zinashiriki michezo hiyo iliyobeba Kauli mbiu "Michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi, Kazi Iendeleee".