Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi nchini kubadilika na kujiandaa kupokea mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni mapendekezo ya wataalamu kutoka katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kudumisha hali ya amani na kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali hapa nchini.
Ametoa rai hiyo leo baada ya kusikiliza kero kutoka kwa wananchi wa eneo la Bububu wakati wa Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika viwanja vya Geji, Shehia ya Kijichi, wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja ambapo awali kabla ya mkutano huo alipata fursa ya kufanya Kikao cha Ndani na Uongozi wa Jeshi la Polisi Visiwani Zanzibar.
“Rais Samia ameanza kuleta mabadiliko makubwa katika vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama, ametoa ajira na kupandisha vyeo Askari akitaka jeshi lishuke chini kwa wananchi ili kuweza kupambana na uhalifu kuanzia ngazi ya Kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya Shehia kwa huku Zanzibar na ndio maana tunaenda kujenga Vituo vya Polisi Kata nchi nzima ili kuweza kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifi”, aisema Masauni.
“Hapa wananchi wamezungumza mambo mengi wakilituhumu Jeshi la Polisi, nawataka Jeshi la Polisi kubadilika katika kupambana na uhalifu, haiwezekani wahalifu tena watoto wadogo wasumbue wananchi, wakati jeshi hili limekua na historia ya kupambana na matukio makubwa ya uhalifu, nawaagiza badilikeni katika kushughulika na uhalifu uliosemwa hapa na wananchi ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani na salama”, aliongeza Masauni.
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pindi jeshi linapowapeleka mahakamani watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya uhalifu huku akisisitiza ulinzi shirikishi kuboreshwa katika jamii.
“Kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi pindi Polisi wanapopeleka watuhumiwa mahakamani hali inayopelekea mahakama kutoendelea na kesi, hapa tuna kesi takribani watu saba wameachiwa hivi karibuni, ni watuhumiwa wa kukata watu mapanga lakini mashahidi hawajatokea mahakamani na sababu kubwa wanalindana na kuogopa kusemwa katika jamii pindi watuhumiwa wakihukumiwa vifungo”, alisema Kamishna Hamad.
Awali akisoma Taarifa ya hali ya uhalifu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Magharibi A, Mary Isungi amesema jumla ya madaraja 13 yameondolewa mahakamani baada ya mashahidi kushindwa kutokea mahakamani huku akikiri hali hiyo inapelekea wahalifu wengi kurudi mtaani na kuendelea na matukio ya uhalifu ikiwemo kuwaingilia watoto kinyume na maumbile, unyang’anyi wa kutumia silaha, kunajisi, kubaka na kuvunja maduka kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi.
Waziri Masauni yupo Visiwani Zanzibar kwa ziara ya kikazi lengo likiwa ni kukagua shughuli mbalimbali pamoja na kuzungumza na Askari Shehia ili kuweza kudhubiti matukio ya uhalifu visiwani humo.