Serikali imeanza kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2004 ili kukidhi mahitaji yaliyopo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameyasema hayo Oktoba 31, 2023 bungeni alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mhe. Stella Ikupa ambaye amehoji mkakati wa serikali kufanya marekebisho ya Sheria namba 9 ya Mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu.
Akijibu swali hilo, Mhe. Katambi amesema mkakati wa serikali kwa sasa ni kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2004 ambapo utekelezaji wake umeanza.
Aidha, amesema baada ya kukamilika kwa mapitio ya Sera ya Mwaka 2004 hatua za marekebisho ya Sheria hiyo zitaanza kwa kuzingatia mapungufu yatakayobainishwa katika tathmini ya utekelezaji wa Sera hiyo.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mhe.Mariam Kisangi amehoji serikali imejipangaje kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ili kutoa maoni kwenye mapitio hayo.
Mhe.Katambi akijibu swali hilo, amesema mapitio ya sera yanatarajiwa kukamilika mwaka huu na yamekuwa shirikishi kwa makundi yote ya watu wenye ulemavu.