Na. Lilian Lundo - MAELEZO
Ushiriki katika Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Saba saba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere Jijini Dar es Salaam, umeendelea kuzipaisha bidhaa za Tanzania baada ya baadhi ya wajasiliamali kupata soko la bidhaa hizo nje ya nchi.
Mmoja wa wafanyabiashara wa korosho, Bi. Sakina Ponella kutoka Mtwara aliieleza hayo leo katika Viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere kuwa ushiriki wake katika maonesho ya mwaka huu umezaa matunda baada ya kupata soko la korosho katika nchi za Ulaya, Asia na Afrika Mashariki.
"Kutokana na ubora wa korosho ninazouza, nimefanikiwa kupata wateja kutoka nchi za Uturuki, China, Syria pamoja na Rwanda," alieleza Bi. Sakina.
Alisema kuwa mmoja wa wateja hao waliotembelea banda lake, amehitaji kutumiwa tani 4000 za korosho kila mwezi lakini kutokana na zao lenyewe kuwa ni la msimu, hivyo amemshauri mteja huyo awe anatumiwa tani nyingi zaidi kipindi cha msimu wa zao hilo badala ya kutumiwa kila mwezi.
Bi. Sakina aliongeza kuwa tayari wamepeana mawasiliano na wateja hao kwa ajili ya hatua ya kuandikishiana mikataba na kuanza kutuma korosho hizo.
Kwa upande wake, Afisa Masoko wa kampuni ya Moringa (Mlonge) Natural Product kutoka Arusha, Leah Moses ameelezea maonesho hayo kuwa yamewasaidia wajasiliamali kujulikana zaidi nje na ndani ya Tanzania.
Alisema kuwa kwa upande wa masoko ya nje amefanikiwa kupata wateja kutoka nchi za Kongo, Kenya na China ambao wamechukua mawasiliano ya kampuni hiyo kwa ajili ya kuagiza bidhaa nyingi zaidi.
Aidha, mfanyabiashara wa vinyago kutoka Mtwara, Bi. Salma Omary amewata wafanyabiashara wadogo wadogo kutumia fursa ya maonesho mbalimbali ya biashara kujitangaza ili kupata masoko ndani na nje ya nchi.
"Wafanyabiashara hawatakiwi kufikiria juu ya kupata faida peke yake katika maonesho kama haya. Lakini wanaweza kutumia fursa ya maonesho ya biashara kwa ajili ya kujitanga zaidi ambapo itawaletea wafanyabiashara wengi zaidi wa kudumu,' alisema Bi. Salma.
Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, yalifunguliwa rasmi Julai 1 mwaka huu na Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Maonesho hayo yalitarajiwa kufungwa Julai 8 mwaka huu. Aidha Rais Magufuli alitoa agizo la kuongezwa siku tano zaidi ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kujitangaza, vile vile kwa Watanzania kujifunza juu ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa.