Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Manyanya: Badilishaneni Uzoefu Katika Mageuzi ya Viwanda.
Dec 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Atley Kuni – OR-TAMISEMI.

Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na uwekezaji Mh. Mhandisi Stella Manyanya amefungua kikao cha siku tatu mjini Dodoma kwa njia ya Mtandao (Video Conferece) huku  akiwataka wataalam katika ngazi ya Mikoa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia mwanya huo kubadilishana uzoefu lakini pia kuibua fursa zilizopo katika maeneo yao katika  uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ifikapo 2025.

Akifungua kikao hicho Manyanya alisema, kupitia fursa ya viongozi hao wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kukutana kwa njia ya Mtandao kutawezesha wote kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mikakati ya ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kwa kupeana taarifa za kujua viwanda vilivyopo katika maeneo yao na maendeleo yake, lakini pia kujua maeneo yaliyotengwa mahususi kwaajili ya viwanda hivyo.

“Mkutano huu utatusaidia pia kupambanua mikakati ya kufufua viwanda vilivyokufa na namna nzuri ya kupata wawekezaji wapya” alisema Manyanya na kuongeza kwamba  lengo la mikutano hiyo ni kuwa na mikakati endelevu ya kujenga uwezo kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri kuhusu masuala ya sekta ya Viwanda, Biashara na uwekezaji.

Manyanya amesema katika awamu ya kwanza Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA), watatoa mafunzo juu usajili wa Biashara, Miliki Ubunifu sambamba na ujenzi wa uchumi wa Viwanda kama falsafa ya Mh. Rais wa awamu ya tano inavyojipambanua kuhusu suala zima la viwanda.

Manyanya ameongeza kuwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Seleman Jafo pamoja na Waziri mwenye dhamana na Viwanda, Biashara na uwekezaji Charles Mwijage, ni viongozi ambao kwa nafasi zao wameonesha nia ya dhati katika kuhakikisha azma iliyowekwa na Serikali ya awamu ya Tano inatimia.

Akihitimisha risala yake ya ufunguzi Mh. Manyanya alisema, Mikutano hiyo ni mwanzo tu, kwani wanatarajia kuwa na chombo imara yaani kuwa na Jukwaa la Uchumi wa Viwanda kama fursa ya kuendelea kuwezesha ujenzi na uendelezaji wa Viwanda Nchini, ambapo wadau watajulishwa tarehe rasmi ya uzinduzi ambao utafanywa na Mh. Waziri Mwijage.

Mkutano huo wa siku tatu kwa njia ya mtandao ulioanza tarehe 18 na kutarajiwa kumalizika tarehe 20 Desemba, 2017 umewakutanisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Elisante Ole Gabriel,  Makatibu Tawala wa Mikoa ya Mbeya, Songwe, Kilimnjaro, na Ruvuma, Mikoa mingine ni  Kigoma, Lindi, Singida na Pwani sambamba na wataalamu wao wa Mikoa na wale wa Halmshauri.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi