Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mama Janeth Magufuli Atoa Zawadi Kwa Wazee Wasiojiweza na Watoto Yatima Zanzibar
Oct 13, 2017
Na Msemaji Mkuu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika kuelekea Kilele cha Mbio za Uhuru mwaka 2017 na Kumbukumbu ya 18 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli leo tarehe 13 Oktoba 2017 amefanya ziara ya kutembelea vituo vya kulelea wazee, watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu mjini Zanzibar.

Akiwa na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein, Mama Janeth Magufuli amekabibidhi zawadi ya  Mchele kilo 7,626, Unga wa Mahindi kilo 7,626, Sukari kilo 1,068 na Mafuta ya Alizeti lita 576, kwa vituo vya kulelea watoto yatima vya Mazizini na SOS pamoja na vituo vya kulelea wazee Welezo  na Sebuleni.

Akizungumza  wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Mama Janeth amesema ameamua kutoa zawadi hizo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, aliyefariki tarehe 14 Oktoba, 1999 ambapo kesho tarehe 14 Oktoba, 2017 taifa litaadhimisha miaka 18 tangu kutokea kifo chake.

Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa akiyahimiza wakati wa uongozi na uhai wake ni kutaka wananchi kuchapa kazi kwa bidii na kujitegemea. Hata hivyo, alitambua kuwa kwenye jamii kuna watu wasiojiweza wenye uhitaji.

Hivyo,  ametoa wito kwa Watanzania, hususan katika kipindi hiki cha kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa,  kujitahidi kumuenzi kwa vitendo kwa kutoa zawadi na misaada mbalimbali kwa watu wenye mahitaji maalum ikiwa ni pamoja na Wazee wasiojiweza, Watoto wanaoishi katika mazingira Magumu, Walemavu, Wagonjwa, Yatima na Wajane.

Mama Janeth pia amewaasa vijana kujiepusha na vitendo viovu ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa upande wake, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, amemshukuru Mama Janeth Magufuli kwa kuwatembelea Wazee na Vijana hao wenye mahitaji maalum na kuiomba jamii nchini kuunga mkono moyo huo wa kujitolea kwa kuwasaidia watu watu wenye mahitaji maalum kama alivyofanya Mama Janeth Magufuli.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi