Skauti Mkuu nchini Bi. Mwantumu Mahiza akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam wakati akielezea sherehe za maadhimisho ya miaka 100 tangu Chama hicho kianzishwe NCHINI. Kulia ni Kamishna Mkuu Msaidizi Mambo ya Nje wa Chama hicho, Bw. Fredrick Nguma na kushoto ni Kamishna Mtendaji wa Skauti Tanzania Bi. Eline Kitaly.
Na Agness Moshi - MAELEZO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 100 ya Chama cha Skauti Tanzania yatakayofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu Cha Dodoma kuanzia tarehe 21 mpaka 29 Julai, mwaka huu.
Skauti Mkuu Tanzania Bi. Mwantumu Mahiza, ameeleza hayo leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ambapo alieleza kuwa maadhimisho hayo yatafungwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Mahiza ametaja Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni kuwa ni: “Kujenga vijana kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya nchi”, lengo likiwa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika kujenga taifa la watu wazalendo na wenye maadili.
Alisema madhimisho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na Skauti 4,000 kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar. Aidha, mkutano huo utakuwa na ugeni kutoka nchi jirani na kutoka Ulaya na Asia.
Skauti Mkuu nchini Tanzania Bi. Mwantumu Mahiza akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam wakati akielezea sherehe za maadhimisho ya miaka 100 tangu chama hicho kianzishwe. Kushoto ni Kamishna Mtendaji wa Chama hicho Bi. Eline Kitaly.
Alisema kuwa ufunguzi wa maadhimisho hayo utaambatana na shughuli mbalimbali kama vile kutoa tunzo za kutukuka kwa viongozi wastaafu wa nchi hii, ambao walikua walezi wa chama cha Skauti nchini kuanzia Awamu ya Kwanza hadi ya Nne kwa Tanzania bara na Zanzibar Awamu zote tano. Tunzo zote hizo zitatolewa na Mgeni rasmi siku ya ufunguzi.
Mahiza ameongeza na kusema: “Chama cha Skauti kitatoa tuzo maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye kwa sasa ni mlezi wa chama cha Skauti Tanzania na atapata tuzo hiyo kwa mujibu wa katiba ya Skauti ibara ya 6 kutokana ujasiri ambao ameonyesha tangu kuingia madarakani.
Alisisitiza kwa kusema, “Hatumaanishi waliotangulia hawakuwa jasiri la hasha, bali Rais amejitolea kwa kujitoa nafsi yake kupambana kwa kila hali kuziokoa rasilimali za Taifa kwa faida ya nchi yetu na kizazi kijacho. Jambo hili analolifanya limepokelewa kwa hisia tofauti katika jamii lakini manufaa ya harakati zake zitanufaisha Taifa kwa karne zijazo”.
Kamishna Mkuu Msaidizi Mambo ya Nje wa Chama cha Skauti Tanzania Bw. Fredrick Nguma (kulia) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea sherehe za maadhimisho ya miaka 100 tangu Chama hicho kianzishwe hapa nchini. Kushoto ni Skauti Mkuu nchini Bi. Mwantumu Mahiza na Kamishna Mtendaji wa Chama hicho Bi. Eline Kitaly.
Ameeleza kuwa namna pekee ya kuunga mkono juhudi za Rais ni kuendelea kuimarisha malezi kwa watoto na vijana kiuzalendo, kijasiri na kimaadili na kuhakikisha wanakua wakithamini rasilimali za nchi kwa kuzitunza, kuziifadhi na kuzilinda.
Skauti kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini kama vile Takukuru, Tume ya Maadili, Kikosi cha Uokoaji na Zimamoto, Wakala wa Misitu Tanzania, Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi, Usalama Barabarani, Taasisi ya Kuzuia Dawa za Kulevya Tanzania na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) watatoa mafunzo ya muda mfupi ili kuwaongezea vijana uwezo na uelewa kwa mambo yanayohusu jamii, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, rushwa, udhibiti wa maambukizi ya ukimwi, maadili, usalama barabarani, lishe bora na kudhibiti moto sehemu mbalimbali.
Chama cha Skauti Tanzania kilianzishwa mwaka 1917 wakati huo ikiitwa Tanganyika katika kijiji cha Magila, Wilaya ya Muheza Moka wa Tanga. Muasisi wa Uskauti ni Lord Baden-Powell, Luteni Jenerali wa jeshi la Uingereza ambaye alikuwa akitoa elimu na mafunzo kwa vijana ili kuwajenga kiuzalendo, kiujasiri, kimaadili na kiukakamavu.