Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 27 Julai 2022 ametembelea na kukagua miradi ya elimu na afya inaotekelezwa katika Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya wasichana kidato cha tano na sita yenye jumla ya majengo 18 inayojengwa katika Kata ya Kajana Kijiji cha kasumo, ujenzi unaogharimu Shilingi bilioni moja. Akiwa katika shule hiyo, Makamu wa Rais ameagiza kuongezwa kwa jengo la maabara ya fizikia ili kukamilisha vema lengo la shule hiyo kuwa mchepuo wa sayansi uliokamilika.
Aidha, Makamu wa Rais amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha wanapanda miti pembezoni mwa shule hiyo ili kupendezesha shule pamoja na kulinda mazingira. Pia amewaagiza kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati pamoja na matumizi sahihi ya fedha. Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kijiji cha Kasumo na Buhigwe kwa ujumla kutumia vema fursa za uwepo wa miradi katika wilaya hiyo kufanya kazi na kujiendeleza kiuchumi.
Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Muyama iliyopo Wilaya ya Buhigwe, Makamu wa Rais amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu bora ya elimu na kuwasihi kujituma katika kupata elimu ili taifa linufaike na viongozi bora pamoja na wataalamu mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kasumo unaogharimu Shilingi milioni 133 ukitarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba 2022. Mradi huo unatekelezwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na serikali.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Kijiji hicho kwa kujitolea katika utekelezaji wa mradi huo na kuwaasa kuendelea kutoa mchango wao katika miradi mingine ikiwemo ya elimu. Amesema ujenzi wa jengo hilo unapaswa kwenda sambamba na nyumba ya watumishi watakaotoa huduma katika zahanati hiyo pamoja na kuhakikisha ujenzi wa eneo la kuchomea takataka unatekelezwa.
Makamu wa Rais amechangia jumla ya mifuko 200 ya saruji pamoja na kuendesha harambee iliopelekea kupatikana kwa mifuko yote 410 inayohitajika katika ujenzi wa zahanati hiyo
Pia, Makamu wa Rais amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buhigwe kupima eneo la ujenzi wa zahanati hiyo na kupatiwa hati ili kudhibiti uvamizi wa ardhi katika eneo hilo.
Wananchi wa Kijiji hicho wameiomba Serikali kujenga nyumba za Walimu katika shule ya msingi Lemba ambayo inakabiliwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu na hivyo kuathiri utoaji wa elimu kijijini hapo.