Na Shamimu Nyaki - WUSM
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maagizo mbalimbali katika Matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika Nyanja mbalimbali ili kuwasaidia Watanzania.
Mhe. Mpango ametoa maagizo hayo katika Kilele cha Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 07,2022 Dar es Salaam, ambapo ameiagiza BAKITA na BAKIZA kuongeza ubunifu katika kuzalisha misamiati bora ya kukuza lugha hiyo.
Ameiagiza Taasisi, Idara na Wakala wa Serikali kutumia lugha ya Kiswahili katika Makongamano, Warsha, Mikutano Mijadala na huduma nyingine.
"Naagiza Mabaraza ya Kiswahili kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha Sheria, Kanuni na Nyaraka mbalimbali ambazo bado hazijatasfriwa kwa kiswahili zinawekwa katika lugha ya kiswahili", amesisitiza Mhe. Mpango.
Aidha, Mhe. Mpango ameagiza Vyombo vya Habari kutumia lugha hiyo kwa ufasaha na kuhakikisha vinapokua na taarifa zilizoandaliwa kwa lugha nyingine zinafanyiwa tafsiri ya kiswahili.
Agizo lingine alilolitoa Mhe. Mpango ni Kwa Balozi za Tanzania Ulimwenguni kuhakikisha zinaazisha Vituo mbalimbali vya kufundisha kiswahili, huku akisisitiza wataalamu wa kufundisha katika vituo hivyo wawe ni wataalamu waliosajiliwa katika Kanzi Data ya BAKITA na BAKIZA.
Mhe. Mpango amesisitiza matumizi sahihi ya Mfumo wa kufundisha kiswahili kwa wageni ili wageni hao wapate urahisi katika kujifunza lugha hiyo.
"Nawahimiza Vijana kuandika na kusoma kiswahili ili tupate Waandishi wengi kama walivyo Marehemu Shaban Robert, Shafi Adam Shafi na wengine ambao watasaidia kueneza lugha hii" amesisitiza Mhe. Philip Mpango.
Awali Makamu wa Rais alitoa pongezi kwa UNESCO kuipa heshima lugha hiyo kuwa na siku yake ya kuadhimishwa ikiwa ni kutambua mchango wa lugha hiyo katika Elimu, kuhimiza Uhuru na Utangamano Afrika.
Amezipongeza pia Dini mbalimbali kwa kutumia lugha ya kiswahili katika vitabu vyao na kuongoza Ibada, huku akizipongeza Nchi za Afrika ambazo zinatumia lugha hiyo akizitaja kuwa ni Msumbiji, Kenya, Uganda, Comorro, Yemen, Oman, Burundi, Rwanda na nyingine.
Ameshukuru pia Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuidhinisha kiswahili kuwa moja ya lugha ya kazi na mawasiliano katika Jumuiya hizo.