Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Azindua SHIMMUTA
Nov 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka viongozi wa Taasisi, Mashirika na Makampuni wanachama wa SHIMMUTA kuhakikisha wanatenga fedha kila mwaka na kuwaruhusu watumishi wao kushiriki michezo hiyo na kutoa kipaumbele kama majukumu mengine muhimu ya kiofisi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi nchini (SHIMMUTA) yanayofanyika katika Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga leo tarehe 20 Novemba, 2022. Pia amewasihi viongozi wa Taasisi, Mashirika na Makampuni Binafsi kuwaruhusu viongozi wa Kamati Tendaji ya SHIMMUTA washiriki kwenye vikao vya uongozi kila inapohitajika kwa maslahi mapana ya wafanyakazi na Taasisi hizo.

Makamu wa Rais amewahimiza viongozi na watumishi katika sehemu za kazi na Watanzania kwa ujumla, kushiriki kwenye michezo, ili kuwa na nguvukazi yenye afya ya mwili na akili ambayo italeta matokeo chanya ya utendaji katika taasisi na kwa maendeleo ya Taifa. Amesema tafiti zinaonesha kuwa michezo ina faida kwa afya ya mwili na akili hivyo husaidia kuondokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu.

Aidha, ametoa wito kwa Taasisi, Mashirika ya Umma na Makampuni Binafsi kuhakikisha wanafanya usafi, kupanda miti na maua katika maeneo yao ya kazi.  Pamoja na kuendelea kushirikiana na Serikali kudhamini Programu mbalimbali zinazohusiana na maendeleo endelevu na utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amekemea vitendo vya taasisi kushirikisha wanamichezo wasiohusika katika michuano hiyo. Aidha ameagiza Baraza la Michezo la Taifa  kufuatilia taasisi 50 ambazo hazijashiriki katika michuano hiyo kwa miaka miwili mfululizo.

Awali akisoma Risala ya Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo ya Mashirika Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi nchini (SHIMMUTA), Roselyne Massam amesema mashindano hayo yameendelea kuwa na mafanikio ambapo kwa mwaka huu zimefika timu 52 kulinganisha na timu 26 mwaka 2018. Amesema changamoto zinazokabili shirikisho hilo ni pamoja na wanachama kutolipa ada kwa wakati na hivyo kukwamisha shughuli za shirikisho.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi