Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Azindua Kiwanda cha Vifungashio Tanga
Nov 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 20 Novemba, 2022 amezindua rasmi kiwanda cha vifungashio cha Yogi Polypack kilichopo Pongwe mkoani Tanga. Ujenzi wa Kiwanda hicho umegharimu Shilingi bilioni 14.1 na tayari kinazalisha mifuko ya kufungishia bidhaa na vyakula vikavu.

Akizungumza mara baada ya kuzindua kiwanda hicho, Makamu wa Rais amewapongeza wamiliki wa kiwanda hicho kwa kuiwezesha Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni ambazo zingetumika kuagiza nje ya nchi bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo. Ametoa wito kwa wananchi wote wenye uwezo wa kuwekeza katika sekta ya viwanda kufanya hivyo na wale wenye viwanda tayari wafanye jitihada za kuongeza uwezo wa uzalishaji ili kukuza uchumi wa taifa.

Makamu wa Rais amesema kiwanda hicho ni mkombozi kwa viwanda vingine na wajasiriamali waliokuwa wakilazimika kuagiza malighafi kutoka nje. Pia ni mwarobaini wa mahitaji ya vifungashio kwa ajili ya mazao ya nafaka, mbegu za mafuta, viazi, parachichi, korosho n.k. ambapo Serikali, makampuni na wakulima walikuwa wanatumia fedha nyingi kuagiza kutoka nje.

Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha juu kwa maeneo ya viwanda mkoani Tanga kupatiwa umeme wa uhakika katika mpango na hatua za muda mfupi za kuimarisha upatikanaji wa umeme zitakazoanza kutekelezwa mwezi Januari 2023.

Pia ameiagiza TAMISEMI kupitia TARURA kushughulikia changamoto ya barabara inayoingia na kutoka katika kiwanda hicho kwa kuwa kiwanda hicho  ni chanzo muhimu  cha mapato ya Serikali Kuu na Halmashauri.

Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa wito kwa wamiliki wa kiwanda hicho kujiwekea malengo ya kutumia malighafi za ndani katika uzalishaji kama katani na mabaki ya bidhaa za plastiki (recycled materials) na kuhakikisha bidhaa za kiwandani hapo ni rafiki kwa mazingira.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amepongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kufuata taratibu zote za kimazingira katika uanzishwaji wake. Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kulinda mazingira mkoani Tanga ikiwemo kutenga eneo maalum la ujenzi wa viwanda pamoja  ujenzi wa Madampo ya kisasa zaidi yaliojengwa mkoani humo.

Awali, akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda cha Vifungashio cha Yogi Polypack, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Rahul Lal ameishukuru Serikali kwa mazingira mazuri ya uwekezaji iliyoweka yanayopelekea vijana wazawa kuwekeza nchini. Amesema kiwanda hicho kimeweza kuajiri wafanyakazi 150 mpaka sasa huku kikitarajiwa kuajiri zaidi ya wafanyakazi 250 kitakapoongeza uzalishaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi