Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaasa wazazi kuzingatia maelekezo ya kitaalamu yanayotolewa na madaktari na wahudumu wa afya ili kuepuka athari zinazoweza kutokana na uzazi ikiwemo vifo vya akinamama na watoto.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa kuzindua Jengo Jipya la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure leo tarehe 13 Septemba 2022, Jengo lililogharimu shilingi bilioni 13. Amewasihi wadau wa lishe hapa nchini pamoja na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za kutoa elimu ya lishe ili akina mama wawe na mimba salama na kuzaa watoto wenye afya njema.
Halikadhalika amewaasa wananchi wa Mwanza na Tanzania kwa Ujumla kuachana na imani potofu kuhusu matumizi ya baadhi ya vyakula na kuhakikisha mama na mtoto wanapata lishe bora kwa manufaa binafsi na Taifa letu kwa ujumla. Amesema akipata lishe bora anaepukana na magojwa ya mara kwa mara na hivyo kuepusha gharama ambazo zingetokana na matibabu.
Aidha, amewataka wahudumu wa afya kujiepusha na vitendo vinavyoharibu sifa njema ya tasnia ya utabibu ikiwa ni pamoja na kutozingatia maadili ya kazi. Amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi hao lakini pia titaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo viovu vinavyoendena kinyume na maadili ya kazi hiyo.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta ya afya na kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza hapa nchini. Aidha ameipongeza sekta binafsi hususani katika huduma za afya kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Amesema Hospitali na vituo vya afya vya mashirika ya dini na watu binafsi vimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini.
Awali akitoa taarifa za Ujenzi wa Jengo hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure Dkt. Bahati Msaki amesema kukamilika kwa Jengo la Mama na mtoto katika hospitali hiyo kumeboresha huduma ya afya katika mkoa wa Mwanza na mikoa Jirani, kumepunguza msongamano katika utoaji huduma kutokana na kuongezeka vitanda hadi kufikia 592 katika hospitali hiyo pamoja na kutarajiwa kupunguza vifo vya Mama na Mtoto.