Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha Miradi ya Ujenzi wanayotekeleza inazingatia ubora, tija, gharama nafuu pamoja na ujenzi wa kisasa unaoendana na wakati ili miradi hiyo idumu kwa muda mrefu na kuwa na tija kwa wapangaji.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 30 Novemba, 2022 wakati wa Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Nyumba 3,500 za Watumishi wa Umma zinazojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma. Ameongeza kwamba ni vyema TBA kufanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji, kuongeza ubunifu na kujenga misingi mizuri ya kujiendesha kibiashara ili kuweza kupata mapato zaidi na kujiendesha pasipo kutegemea ruzuku kutoka Serikalini.
Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuharakisha mchakato wa marekebisho ya kanuni ya Uanzishwaji wa Wakala wa Nyumba Tanzania ili Taasisi iweze kukamilisha taratibu zote za kuingia ubia na wawekezaji hali itakayopunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali pekee katika kutekeleza miradi mikubwa nchini na pia itatatua changamoto ya kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi hiyo.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewataka TBA kuweka utaratibu shirikishi kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao katika maeneo ya nyumba hizo. Pia amewasihi Watumishi wa Umma watakaopangiwa nyumba hizo kuzitunza na kuhakikisha zinabaki katika hali ya ubora wake ikiwemo kuzingatia masuala ya usafi na utunzaji mazingira.
Makamu wa Rais amesema uwekezaji katika sekta ya ujenzi ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaendelea kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kama ilivyopangwa. Aidha, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono ubunifu na mipango ya Taasisi kama TBA kuwa na miradi mingi zaidi ya ujenzi ili kuongeza makusanyo ya ndani na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema mradi huo utapunguza changamoto kubwa ya makazi ya watumishi wa umma waliopo jijini Dodoma pamoja na ukuzalisha ajira kwa wananchi wanaozunguka mradi huo.
Profesa Mbarawa ameongeza kwamba ujenzi wa mradi huo unasaidia Wataalamu wazawa wa fani za ujenzi kujengewa uwezo wa taaluma kwa vitendo pamoja na kusaidia kuendelea kukua kwa kasi kwa Jiji la Dodoma lililopangwa vizuri kwa kuzingatia mipango miji, kuongezeka kwa mapato ya serikali na huduma za kijamii katika jiji hilo.
Awali akitoa taarifa za ujenzi wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daudi Kandoro amesema tayari Serikali imetoa fedha za utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo kiasi cha Shilingi bilioni 14.3 pamoja na kutoa Shilingi bilioni 1 katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo wa nyumba nyingine 150 ambapo maandalizi yake yameshaanza.
Kandoro amesema TBA inaendelea kutekeleza miradi mingine nchi nzima kwa fedha za ruzuku na makusanyo ya ndani ikiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba mpya 20 za Viongozi katika eneo la Kisasa Dodoma, ukamilishaji wa nyumba za Majaji kwenye Mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Shinyanga, Tabora na Kagera, ukarabati wa nyumba za makazi ya watumishi wa Umma na Viongozi Tanzania Bara ili kuwawezesha kuishi katika mazingira bora, ujenzi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma katika eneo la Magomeni Kota na Temeke Kota, Ujenzi wa jengo la makazi eneo la Masaki, ujenzi wa nyumba 13 za watumishi mikoani, umaliziaji wa jengo la makazi la ghorofa 11 lenye uwezo wa kuchukua familia 22 Mtaa wa Simeoni Arusha.