Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Aweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Butimba
Sep 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaasa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla kuchukulia kwa umuhimu suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kuepukana na mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kusababisha kupotea kwa vyanzo vya maji.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 14 Septemba, 2022 mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Chanzo cha Maji na Kituo cha Tiba ya Maji cha Butimba uliopo Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, mradi unaogharimu Shilingi bilioni 69.3 ukitarajiwa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku na kuhudumia watu 450,000 wa Jiji la Mwanza. Amesema ni lazima zifanyike juhudi za ziada katika kupanda miti ambayo ni rafiki kwa mazingira na kuondokana na kufanya shughuli za kiuchumi kandokando mwa vyanzo vya maji ambazo huchangia kupungua kwa rasilimali za maji na hivyo kusababisha ukame.

Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Misitu (TFS), kutoa elimu ya upandaji miti kwa wananchi na katika maeneo inayotekelezwa miradi mbalimbali nchi nzima ili kuendana na miti Rafiki kwa mazingira na vyanzo vya maji.

Pia amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanakuwa na Idara ya Mazingira katika maeneo yao pamoja na watumishi wenye weledi wa kutosha katika masuala ya mazingira pamoja na idara hizo kupewa bajeti katika kutekeleza majukumu yao.

Pia, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Maji kukamilisha mradi huo ifikapo mwezi Desemba mwaka huu ili kuondoa adha ya upatikanaji maji wanayoipata wananchi wa Mwanza licha ya uwepo wa ziwa Victoria katika ukanda wao. Ameigiza Mamlaka za Maji kutotumia siku zaidi ya saba katika kuwaunganishia wananchi huduma za maji pamoja na kuacha mara moja utoaji wa bili zisizo halali kwa watumiaji wa huduma za maji.

Halikadhalika amewataka wafanyakazi waliopata ajira katika mradi huo kuwa waaminifu na kujiepusha na vitendo vya wizi wa vifaa vya ujenzi ili kurahisisha mradi huo kukamilika kwa wakati. Makamu wa Rais ameagiza wafanyakazi hao kupata maslahi yao kwa wakati muda wote wanapofanya kazi katika mradi huo.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema licha ya uwepo wa mradi huo jijini Mwanza, pia Serikali kupitia Wakala wa Maji Vijiji (RUWASA), inatekeleza miradi 45 mkaoni Mwanza yenye jumla ya gharama ya Shilingi bilioni 105 ili kuhakikisha maeneo ya pembezoni wanapata maji safi na salama yanayotosheleza. Aidha Aweso amesema tayari wizara imepokea mitambo ya uchimbaji visima inayotarajiwa kutolewa kila mkoa na hivyo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akitoa salamu za Mkoa ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa miradi ya maji katika Mkoa wa Mwanza na kuahidi kusimamia kikamilifu miradi hiyo kuhakikisha inatekelezwa katika viwango vilivyowekwa. Amesema ili kuhakikisha miradi ya maji hususani ya vijijini inakua endelevu, mkoa una jumla ya jumuiya za watumiaji wa maji 40 ambazo zitasaidia kusimamia miradi ya maji vijijini kwa misingi endelevu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi