Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Atoa Salamu za Serikali Baada ya Ibada ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwl. Nyerere
Oct 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Eatanzania kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo ikiwemo kufanya kazi kwa bidii pamoja na kupinga vikali Rushwa.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Ibada maalum ya kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki Mjini Bukoba mkoani Kagera leo tarehe 14 Oktoba, 2022.

Amesema katika kumuenzi Hayati Baba wa Taifa ni lazima kuendelea kusisitiza amani na umoja kwa Watanzania pamoja na bara la Afrika kwa ujumla.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi kuendelea kufanya kazi kwa kutenda haki, kufanya kazi kwa uadilifu na kuondokana na Rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Makamu wa Rais amewaasa Watanzania kufanya bidii katika masomo ili taifa liweze kupata wataalamu watakaotoa msaada katika mambo mbalimbali nchini.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa Watanzania kutafuta hekima za Mwenyezi Mungu wakati wote wa kutekeleza majukumu kama alivyofanya Hayati Baba wa Taifa enzi za uhai wake.

Ibada maalum ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere imeongozwa na Askofu wa Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango pamoja na Mkewe Mama Mbonimpaye Mpango, Familia ya Baba wa Taifa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere, Mawaziri mbalimbali, Mkuu wa Mkoa Kagera , Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na Vyama vya Siasa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi