Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa kuongeza tija katika ukusanyaji mapato hasa kwa kujenga mifumo rafiki ya kielektroniki itakayowezesha kukusanya mapato bila urasimu pamoja na kusimamia matumizi sahihi ya mapato hayo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 36 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika Jijini Mbeya kuanzia tarehe 12 hadi 14 Septemba, 2022. Amesema viongozi wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za mapato na wanashirikishwa katika matumizi ya fedha hizo.
Aidha, Makamu wa Rais amewaasa Madiwani na wenyeviti wa Halmashauri kuwa mstari wa mbele katika kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya fedha za miradi zinazotolewa katika halmashauri. Pia amewasihi madiwani kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kuhakikisha Sheria na kanuni za manunuzi zinafuatwa pamoja na thamani ya fedha halisi katika miradi mbalimbali inaonekana.
Pia, amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano na kuepusha migogoro ambayo imetawaliwa na maslahi binafsi baina ya viongozi na hivyo kuchelewesha shughuli za maendeleo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka viongozi hao kusimamia kikamilifu katazo la Serikali la kupiga marufuku vifungashio vya plastiki na kuhakikisha oparesheni za mara kwa mara za usafi zinafanyika katika maeneo yote nchini.
Amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapaswa kuendelea kutoa elimu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya uhifadhi wa mazingira pamoja na kusambaza vyombo vya kutupia takataka katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu.
Vile vile, Makamu wa Rais ameitaka Wizara husika ya Mazingira kwa kushirikiana na TAMISEMI kufuatilia utekelezaji wa malengo yaliowekwa katika Serikali za Mitaa ikiwemo kupanda miti milioni 1.5.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema mkutano huo ni muhimu kwa maslahi ya halmshauri na taifa kwa ujumla ambapo unalenga kujadili masuala yote muhimu ya msingi yenye maslahi kwa wananchi.
Aidha, amesema TAMISEMI imeongeza maoteo ya makusanyo ya mapato kutoka Shilingi bilioni 800 hadi Shilingi trioni 1.03 mara baada ya mafanikio iliopta katika ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Amewataka viongozi wote wa Halmashauri kuendelea kusimamia halmashauri kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuhamasisha na kusimamia wananchi katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuwa na miradi endelevu.
Dkt. Dugange amesema kwamba TAMISEMI imeandaa mifumo ya kielektroniki ya utoaji na ufuatiliaji wa mikopo na kuagiza mikopo hiyo kutolewa kwa wahusika na si vinginevyo pamoja na kurejeshwa kwa wakati.
Awali Mwenyekiti wa ALAT, Murshid Ngeze amesema mkutano huo umelenga kujadili utekelezaji wa kazi za Jumuiya kuongeza tija katika ukusanyaji mapato pamoja na matumizi bora ya mapato.
Amesema ushirikiano wa Kimataifa wa Jumuiya hiyo umepelekea kupatikana kwa ufadhili wa miradi mbalimbali ambapo tayari Serikali ya Morocco imekubali kushirikiana na Halmashauri za Tanzania katika utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi.