Januari 5, 2022, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametembelea na kukagua zoezi la upandaji miti na uhifadhi wa Bonde la Mzakwe lililopo mkoani Dodoma.
Akikagua uhifadhi wa bonde hilo ambalo pia ni chanzo cha maji , Makamu wa Rais ameoneshwa kutoridhishwa na usimamizi na ufuatiliaji wa uhifadhi wa bonde hilo uliopelekea kupotea kwa miti iliyopandwa hapo awali kutokana na moto uliotokea Novemba, 2021 pamoja na baadhi ya miti mingine kushindwa kustawi.
Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa Wakala wa Misitu (TFS) pamoja na Mkoa wa Dodoma kushirikisha jamii katika uhifadhi ili wananchi watambue umuhimu wa miti hiyo pindi inapopandwa katika maeneo yao.
Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kuwa na uhakika wa aina ya miti inayoweza kustawi katika bonde hilo ikiwemo miti ya asili. Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuainisha miti inayopandwa pamoja na malengo yake ili kuepusha miti inayoweza kuwa chanzo cha kupoteza maji na ile itakayoshindwa kustawi katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewaasa viongozi wa Mkoa wa Dodoma kuangalia Sheria ndogondogo zitakazowezesha wananchi kupanda miti hasa katika maeneo ya makazi na ya biashara ili kutunza mazingira na kuongeza uwezekano wa upatikanaji mvua kwa wingi mkoani humo.
Dkt. Mpango amesema utekelezaji wa kampeni ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani ni wajibu wa kila Mtanzania na kuwaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, Watendaji wa Kata na Vijiji kuongoza zoezi la upandaji miti na kuisimamia kikamilifu.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi walioshiriki ziara hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga amesema maelekezo yote yaliotolewa na Makamu wa Rais yatafanyiwa kazi kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha zoezi la kuifanya Dodoma kuwa ya kijani. Amesema tayari mkoa huo umeandaa miche milioni mbili na tayari maandalizi yamefanyika katika taasisi zote zilizopo mkoani humo ili zikabidhiwe miche hiyo.