Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaasa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na kanda ya ziwa kwa ujumla wanaojishughulisha na uvuvi kuacha kutumia dawa zisizofaa katika uhifadhi wa Samaki ili kuepukana na ongezeko la wagonjwa wa saratani katika mkoa huo.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 13 septemba 2022 wakati akizindua Jengo la Wodi ya Wagonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando iliopo Jijini Mwanza. Amezitaka mamlaka za udhibiti kuhakikisha wanakomesha jambo hilo mara moja.
Makamu wa Rais amesema Serikali inawekeza katika ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha huduma za matibabu ya saratani zinasogezwa karibu na wananchi. Ameongeza kwamba takwimu zinaonesha kuwa ugonjwa wa saratani bado ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza duniani kwa kusababisha vifo kwa watu wengi ambapo nchini Tanzania takribani watu 42,000 kila mwaka hupata ugonjwa huo wa saratani.
Makamu wa Rais amelishukuru Kanisa Katoliki na Madhehebu mengine kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kusogeza huduma za jamii ikiwemo afya karibu na wananchi. Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wengine ili kuendelea kuboresha huduma za afya hapa nchini.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanzisha kiwanda cha mionzi dawa kitakachosaidia utoaji huduma kwa wagonjwa wa saratani.
Aidha Dkt. Mollel amewaasa viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao kuwa na bima za afya kwa usalama wa afya zao pamoja na kuwa na uhakika wa mapato ya kuendesha vituo vya kutolea huduma za afya.
Awali akitoa taarifa za Ujenzi wa Wodi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dkt. Fabian Massaga amesema kukamilika kwa Jengo hilo kumeleta unafuu mkubwa kwa wananchi wa kanda ya ziwa ambao wanapata huduma za matibabu, kupungua kwa gharama za wagonjwa waliokuwa wakipata malazi kutoka nje ya hospitali pamoja na wagonjwa kufuatilia huduma za tiba kwa usahihi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Hospitali ya Bugando, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mwanza Mhashamu Renatus Nkwande, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendeleza ushirikiano na kanisa hilo katika kuhudumia wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya.
Amesema ujenzi wa Jengo hilo utaokoa Maisha ya watu wengi wanaokubwa na madhila ya saratani ndani na nje ya Tanzania. Askofu Nkwande ameiomba serikali kuisaidia hospitali hiyo kupata mashine, vifaa pamoja na samani zitakazorahisisha katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa saratani.