Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Akishiriki Mkutano wa SADC Angola
Aug 17, 2023
Makamu wa Rais Akishiriki Mkutano wa SADC Angola
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Intercontinental Jijini Luanda nchini Angola leo tarehe 17 Agosti, 2023
Na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 17 Agosti, 2023 amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Intercontinental, Jijini Luanda nchini Angola. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akijadiliana jambo na baadhi ya viongozi wa ujumbe wa Tanzania wakati wa Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Intercontinental Jijini Luanda nchini Angola leo tarehe 17 Agosti 2023. (Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Balozi Kennedy Gaston pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Jamal Kassim Ali).

 

Mkutano huo uliobeba kaulimbiu ya “Umuhimu wa Rasilimali Fedha na Rasilimali Watu katika kuendeleza Viwanda na Uchumi” umehudhuriwa na viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya hiyo, Mawaziri, Viongozi wa Kisekta pamoja na Wakuu wa Majeshi. Baadhi ya masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na uendelezaji viwanda kwa kuhakikisha uongezaji thamani wa bidhaa unafanyika ndani ya nchi wanachama ili kuongeza ajira na mapato kwa mataifa husika. Pia, Tanzania imesisitiza umuhimu wa usalama wa chakula pamoja na umuhimu wa kutafuta amani kwa nchi za Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

 

Katika Mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi amekabidhi Uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Jamhuri ya Angola Mhe. João Lourenço. Pia, Rais wa Namibia Dkt. Hage Geingob amekabidhi Uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC Organ Troika) kwa Rais wa Zambia Mheshimiwa Hakainde Hichilema.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 43 wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Intercontinental Jijini Luanda nchini Angola leo tarehe 17 Agosti 2023. 

 

Mkutano huo, umetoa zawadi mbalimbali kwa washindi wa shule za sekondari wa shindano la insha la Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) ambapo Mwanafunzi Hollo Kadala  wa shule ya sekondari Msalato kutoka nchini Tanzania ameshinda nafasi ya tatu.

 

Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali umetanguliwa na mkutano wa Kamati ya Baraza la Mawaziri la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 13–14 Agosti 2023.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi